1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump akimbizwa jukwani Nevada na maafisa usalama

6 Novemba 2016

Mrepublican Donald Trump alitolewa jukwaani wakati wa mkutano mjini Reno,Nevada, kufuatia kitisho cha usalama wakati yeye na Mdemokrat Hillary Clinton wakiwinda kura katika majimbo muhimu kuelekea uchaguzi wa Jumanne.

USA Reno Präsidentschaftskandidat Donald Trump und Sicherheitsdienst
Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Locher

Kitisho hicho hakikuwa bayana. Maafisa wawili wa usalama walimkamata Trump kwa mabega na kumvuta nyuma ya jukwaa wakati maafisa wa polisi wakimvamia mwanaume wa kizungu mbele ya umati na kumuweka uso sakafuni huku wakimkagua. Muda mfupi baadae, mwanaume huyo alisindikizwa na polisi mikono nyuma, na Trump, akionekana mtulivu, alirejea jukwaani na kuendelea na kampeni yake. "Hakuna aliesema itakuwa rahisi kwetu," alisema. "Lakini kamwe hatutazuiwa."

Tukio hilo lilianza wakati Trump alipobaini mtu aliemdhania kuwa mzomeaji, akisema alikuwa mtu "kutoka kambi ya Clinton." Sekunde chache baadae watu waliokuwa karibu na jukwaa walianza kumnyooshea vidole mtu aliekuwa miongoni mwa watu wa karibu na jukwaa. Kisha maafisa usalama walimuondoa Trump. Ripota wa CNN aliezungumza na mashuhuda katika tukio hilo alisema hakuna alieona silaha. Idara ya usalama pia ilitoa taarifa na kusema mtu aliekamatwa hakuwa na silaha.

Tukio hilo lilitokea wakati Clinton na Trump wakiwasilisha hoja zao za mwisho mwisho kwa wapigakura wa Marekani, wakiizunguka nchi katika matumaini ya kuwavutia wapigakura ambao bado hawajaamua wa kumchagua, na kuhamasisha ngome zao kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi.

Mjini Philadelphia, mwanamuziki wa miondoko ya pop Kate Perry alitumbuiza katika mkutano wa Clinton, akiwa wa karibuni zaidi katika mkururo wa nyota wanaoungana na mgombea huyo kwa lengo kupata kura kutoka kwa vijana. "Wakati watoto wako na wajukuu zako watakapokuuliza ulifanya nini mwaka 2016 wakati kila kitu kilikuwa hatarini, nataka uwe na uwezo wa kusema kuwa ulipiga kura kwa ajili ya Marekani iliyo bora na imara zaidi," alisema Clinton.

Uchunguzi wa maoni unaonyesha Clinton bado ana nafasi katika majimbo yanayoweza kuwa muhimu katika kuamuwa matokeo ya uchaguzi huu. Lakini uongozi wake umepungua baada ya ufichuzi wiki iliopita kwamba shirika la upelelezi FBI, lilikuwa linakagua rundo la barua pepe mpya kama sehemu ya uchunguzi wake wa namna alivyoshughulikia taarifa nyeti wakati akiwa waziri wa mambo ya kigeni.

Mwanaume akisindikizwa na maafisa usalama muda mfupi baada ya mgombea wa Republican Donald Trump kuondolewa jukwaani katika mkutano wa kampeni mjini Reno, Nevada, Jumamosi usiku.Picha: picture-alliance/AP Photo/ E. Vucci

Matokeo ya uchunguzi wa maoni ulioendeshwa na mashirika ya McClatchy na Marist yaliotolewa siku ya Jumamosi yalionyesha Clinton akiongoza kwa pengo la asilimia moja ikilinganishwa na asilimia 6 mwezi Septemba. Nao uchunguzi wa Reuters na Ipsos siku hiyo hiyo ya Jumamosi ulionyesha Clinton akiwa mbele kwa tofauti ya asilimia 4 kitaifa ikilinganishwa na asilimia 5 aliokuwa nayo siku ya Ijumaa.

Mashindano ya kura za Florida

Wagombea wote wawili walitumia muda jimboni Florida, linalochukuliwa kuwa moja ya majimbo yanayogombaniwa sana. Uchaguguzi wa mwaka 2000 uliamuliwa jimboni Florida, baada ya mgogoro juu ya kura na kuhesabiwa upya kura kufikishwa katika mahakama kuu ya Marekani, ambayo ilimpa ushindi Mrepublican George W. Bush dhidi ya Mdemokrat Al Gore.

Uchunguzi wa kura za maoni katika jimbo hilo ulibaini Clinton alikuwa akiongoza kwa tofauti ya asilimia 1 tu, hii ikiashiria kuwa mpambano katika jimbo hilo ni mkali sana. Trump alizungumza katika mkutano mjini Tampa, Florida Jumamosi asubuhi, ambako aliendelea kumkosoa Clinton kwa kuunga mkono mpango wa bima nafuu ya afya -- maarufu kama "Obama Care", baada ya kutolewa tangazo kwamba malipo yataongezeka mwakani. "Haitajalisha kwa sababu nikishinda nitaufutilia mbali," alisema Trump.

Muda mfupi kabla Clinton hajapanda jukwaani mjini Pembroke Pines, jimboni Florida, mvua ilinyesha. Watu waliokuwa wanamsubiri mgombea huyo katika eno la wazi walibakia na kusubiri, wakitoa miavuli na wengine kujifunika mifuko ya plastiki inayotumika kukusanya taka. "Nimevutiwa kuwa hapa na kundi hili maridhawa, ije mvua au jua mko tayari," alisema Clinton. Lakini alifupisha hotuba yake baada ya kulowa na mvua akisema," Sidhani kama nahitaji kuwaambia mambo yote mabaya kuhusu Donald Trump."

Katika maktaba ya JFK mjini Hialeah, Florida, watu walipanga foleni nje kwa ajili ya uchaguzi wa mapema. Eneo la karibu na hapo wafuasi wa wagombea wote walikuwa wakipeperusha vibao na kuimba nyimbo, wakiwataka madereva waliokuwa wakipita kupiga honi. "Tunahitaji mtu aingie na kusafisha nyumba," alisema raia wa Marekani mwenye asili ya Cuba Ariel Martinez mwenye umri wa miaka 42, na mfuasi wa Trump.

Uchaguzi wa mapema ulianza Septemba na kampuni ya Catalist, inakadiria kuwa zaidi ya kura milioni 30 zimepigwa katika majimbo 38. Kuna takribani watu milioni 225.8 wenye vigezo vya kupiga kura nchini Marekani. Jumamosi ndiyo ilikuwa siku ya mwisho ya upigaji kura wa mapema katika kaunti nyingi za Florida.

Mabadiliko ya mipango

Timu za kampeni za Trump na Clinton zilibadili ratiba za usafiri wa wagombea hao kwa siku mbili zijazo kwenda kwenye majimbo wakaona  fursa. Trump aliwaambia watu mjini Tampa kwamba kungekuwa na mkutano wa kampeni mjini Minnesota mwishoni mwa wiki hii. Minnesota haijawahi kuchaguwa mgombea wa Republican tangu 1984. Kampeni yake ilithibitisha mkutano uliokuwa umepangwa kufanyika Wisconsin siku ya Jumapili umefutwa.

Wafuasi wa wagombea wa vyama vya Democratic (kushoto) na Republican (kulia) wakiwashabikia wagombea wao katika mikutano yao ya kampeni.Picha: picture-alliance/AP Photo/R. D. Franklin/ G. Herbert

Clinton alianza siku kwa kusimama katika kituo cha kijamii cha Miami Magharibi, eneo la Wamarekani wenye asili ya Cuba akiwa pamoja na nyota wa telenovela Jencarlos Canela, mwenyeji wa Miami mwenye asili ya Cuba.

Baadae alitembelea ofisi ya kampeni yake mjini Little Haiti ambako kuna wakaazi wengi raia wa Marekani wenye asili ya Haiti. Clinton aliungana na Sybrina Fulton, mama yake Trayvon Martin, kijana mweusi ambaye hakuwa na silaha wakati aliuawa mwaka 2012 na mlinzi wa kijiji cha Florida George Zimmerman.

Wakati Trump akipendelea mikutano mikubwa mikumbwa, Clinton amejaza ratiba zake za kampeni na mikutano ya shabaha iliyolengwa kuwavutia wapigakura katika demografia makhsusi. Wapigakura wenye asili ya Cuba wamekuwa wakiwapendelea Warepublican kihistoria, lakini vizazi vya sasa vimehamia kwa wagombea wa chama cha Democratic.

Katika kile kinachoonekana kuwa ni juhudi za kulinda ngome za Democratic, Clinton atapiga kampeni siku ya Jumatatu katika mji wa Grand Rapids, Michigan, kabla ya kurejea Pennsylvannia kwa ajili ya mkutano mjini Philadelphia pamoja na rais Barack Obama na mke wake Michelle Obama, na rais wa zamani Bill Clinton.

Trump atasimama Jumapili katika majimbo ya Iowa, Minnesota, Michigan, Pennsylvania na Virginia kujaribu kunyakuwa baadhi ya majimbo ambayo yamekwenda kwa Wademocrat katika chaguzi za karibuni za rais.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre

Mhariri: Bruce Amani