Trump akutana na Obama
11 Novemba 2016Wakati maandamano dhidi ya rais mteuele tajiri mfanyabiashara ya kuuza majumba kutoka chama cha Republican yalirindima katika miji ya Marekani na miji mikuu ya nchi mbali mbali duniani ikitafakari na hali ya sintofahamu inayoikabili dunia, Obama na Trump waliahidi kuendelea na utaratibu usiokuwa na matatizo wa kupokezana madaraka.
Baada ya kampeni iliyokuwa na kila hali ya uhasama ambayo ilimalizika kwa kuchaguliwa kwa bilioanea mwenye umri wa miaka 70 na nyota wa zamani katika televisheni ambaye hajawahi kushika wadhifa wa uongozi wa umma na ambaye alipata madaraka kwa kampeni za sera za mrengo wa kulia, ujumbe ulikuwa: mambo hapa yanakwenda kama kawaida yake katika demokrasia.
Rais anayeondoka madarakani na mrithi wake walikuwa na mazungumzo ya ana kwa ana katika ofisi kuu ya rais , Oval Office, kwa kile Obama alichokieleza kuwa ni mazungumzo mazuri, na tena alionekana kuwa katika hali ya kawaida kabisa hadharani.
"Nimetiwa moyo sana nafikiri na hamasa ya rais mteule Trump akitaka kufanyakazi na timu yangu , kuhusu masuala mengi ambayo nchi hii muhimu inayakabili".
Mkutano huo ambao umekuja chini ya masaa 36 baada ya ushindi wa kushitua wa Trump dhidi ya mgombea wa chama cha Democratic Hillary Clinton, ulikuwa na uwezo wa kuwa wa shaka shaka.
Kwa kuwa , Trump aliongoza kile kinachojulikana kama vuguvugu la uzawa, likipinga kwamba Obama alizaliwa nchini Marekani, wazo ambalo linaonekana kuwa na dhamira ya ubaguzi, na aliachana na mtazamo huo hivi karibuni.
Rais mjivuni
Na iwapo rais mteule atatekeleza kila ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni, ataondosha karibu kila mafanikio ya Obama yalipo. Trump hivi karibuni alimuita Obama , "rais mwenye majivuno mno katika historia ya nchi hiyo" , alisema anamatumaini ya kupata ushauri wa rais.
"Tumejadiliana kuhusu hali mbali mbali, baadhi nzuri sana na baadhi zenye matatizo. Nina matumaini makubwa ya kufanyakazi na rais hapo baadae ikiwa ni pamoja na ushauri".
Wakati waume zao wakifahamiana , mke wa rais , Michelle Obama pia alikutana na mrithi wake Melania Trump ikulu ya White House. makamu wa rais Joe Biden , wakati huo huo , alikutana na mgombea mwenza wa Trump , Mike ence, ambaye ndie makamu mpya wa rais.
Maandamano pia yaliendelea katika mitaa ya miji ya Marekani kupinga kuchaguliwa kwa Doland Trump kuwa rais. Katika pwani ya mashariki, waandamano yalifanyika mjini Washington, Baltimore, Philadelphia na New York , wakati upande wa pwani ya magharibi waandmanaji waliingia mitaani mjini Los Angeles, San Francisco na Oakland , Califonia, na Portland, Oregon. Maandamano hayo kwa kiasi kikubwa yalikuwa ya amani , licha ya kuwa kulikuwa na vitendo vya hapa na pale vya ghasia.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre
Mhariri: Daniel Gakuba