1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump akutana na Papa Francis

24 Mei 2017

Rais wa Marekani Donald Trump amekuatana na kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis. Viongozi hao mashuhuri ulimwenguni ambao mara nyingi hawakubaliani katika mambo kadhaa wamekutana kwa mara ya kwanza

USA Trump Family beim Papst Gruppenfoto
Picha: Reuters/A. Tarantino

Mkutano huo wa faragha ulidumu kwa dakika ambazo hazikutimia 30 ulimalizika kwa viongozi hao kupeana mikono mbele ya kamera za waandishi wa habari huku rais wa Marekani Donald Trump akimshukuru papa Francis na kumwambia kuwa amefurahi sana na kwamba hiyo ilikuwa ni heshima kubwa aliyopewa kuweza kufika Vatican.  Ziara ya Trump ilipangwa katika muda mchache hali iliyosababisha kubadilika mpangilio wa kazi wa kiongozi wa kanisa Katoliki Duniani mwenye umri wa miaka 80, Papa Francis.

Huu ni mkondo wa tatu katika safari ya kwanza ya nje ya rais wa Marekani Donald Trump ambapo amezitembelea Saudi Arabia, Israel na Mamlaka ya Palestina.  Trump na Papa Francis wana historia ambayo kwa kiasi kikubwa inatia hamu kutaka kuijua.  Kwanza hawakubaliani na wamepingana hadharani katika maswala yanayohusu uhamiaji, uchu unaoletwa na ubepari, maswala ya mabadiliko ya tabia nchi, adhabu ya kifo na biashara ya silaha.  Lakini wote wawili wanapinga juu ya kuhalalisha utoaji mimba. Katika ziara hiyo, rais wa Marekani aliandamana na mkewe Melania, binti yake Ivanka na mumewe Jared Kishner, msaidizi mkuu wa White House na mshauri wa maswala ya usalama Mcmaster.  Baada ya kumalizika mkutano shuguli ya kupeana zawadi ilifuata.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa FrancisPicha: Reuters/A. Bianchi

Papa Francis alifanya mazungumzo na wageni wake kwenye maktaba yake binafsi iliyopo katika ikulu ya Vatican ambayo huwa haitumii mara nyingi. Rais wa marekanim Donald Trump baada ya kukutana na papa Francis alipanga kumpigia simu rais wa Italy Sergio Mattarella na waziri wake mkuu Paolo Gentiloni. Bibi Melania atazuru hospitali ya watoto na Ivanka Trump atafanya mazungumzo na wawakilishi wa jamii wa kidini wa St. Egidio, wanatarajiwa kujadili juu ya maswala yanayohusiana na uhamiaji na usafirishaji watu kinyume cha sheria.

Trump na timu yake baadae watasafiri kuelekea Ubelgiji kwa ajili ya kukutana na maafisa wa Umoja wa Ulaya na wa Jumuiya ya kujihami ya NATO kabla ya kurejea Italia hapo kesho ili kuhudhuria mkutano mkuu wa nchi za G7 utakaofanyika katika mji wa Sicily siku ya Ijumaa na Jumamosi.

Mwandishi:  Zainab Aziz/AFPE/APE

Mhariri: Mohamed Abdulrahman

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW