Trump aanza ziara ya siku nne Mashariki ya kati
13 Mei 2025
Baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mfalme Khalid, Donald Trump amepokelewa na Mwanamfalme Mohammed bin Salman, aliyemuhakikisha kwamba Saudi Arabia itabakia kuwa mshirika wake imara.
Kama sehemu ya kuonesha heshima, ndege za kijeshi za Saudi Arabia zilionekana zikiisindikiza ndege ya Rais wa Marekani Airforce One ilipokaribia mji mkuu Riyadh.
Soma zaidi: Nchi za Kiarabu zatumaini biashara na Marekani licha ya vita vya Gaza
Trump na Mwanamfalme bin Salman wameandaliwa kushiriki chakula cha mchana katika dhifa maalumu sambamba na wafanyabiashara wakubwa walioalikwa wakiwemo Mkurugenzi mkuu wa Kampuni ya Blackstone Stephen Schwarzman, Larry Fink wa BlackRock na Elon Musk.
Anatarajiwa pia kufanya mkutano wa uwekezaji kati ya Marekani na Saudi Arabia kabla ya kuelekea Umoja wa Falme za Kiarabu na Qatar katika ziara yake ya siku nne kwenye mataifa hayo ya ghuba.
Viongozi wa Kuwait, Oman na Bahrain kukutana na Trump
Kando ya viongozi wa Saudia, kesho Jumatano kiongozi huyo wa Marekani anatazamiwa kukutana na viongozi wa Kuwait, Oman na Bahrain. Mazungumzo yake mjini Riyadh yanayotazamiwa kulenga zaidi mikataba ya kibiashara kuliko masuala ya kidiplomasia huenda yakazaa matunda kwa kupata makubaliano na Saudi Arabia kuhusu teknolojia ya nyuklia.
Nchi hiyo tayari imeshatangaza kuwa itawekeza dola za Kimarekani bilioni 600 nchini Marekani katika miaka ijayo wakati Trump amesema atamwomba Mwanamfalme Salman kiasi hicho kiongezwe hadi kufikia dola trilioni moja.
Saudi Arabia ilikuwa pia nchi ya kwanza kwa Trump kuitembelea alipoingia madarakani katika awamu yake ya kwanza mnamo mwaka 2017 baada ya nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa mafuta kutangaza kuwekeza dola bilioni 450 Marekani.
Wakati suala la mpango wa nyuklia ya Iran likitarajiwa kuwa katika orodha ya ajenda za mazungumzo ya Trump katika ziara hiyo, Iran imetoa onyo. Kituo cha habari cha Nournews cha nchini humo kimemnukuu mkuu wa utumishi katika jeshi Mohammad Bagheri akisema Saudi Arabia inapaswa kutokuegemea upande wowote. Ameongeza kuwa uchokozi wowote dhidi ya Iran kwa hakika utasababisha Iran ilipe kisasi.