Trump amfuta kazi mkuu wa usalama wa mitandao
18 Novemba 2020Rais Donald Trump alitangaza katika mtandao wake wa Twitter siku ya Jumanne kwamba, amemfuta kazi Chris Krebs mkurugenzi wa shirika la usalama na miundombinu nchini Marekani CISA.
CISA, ambayo iko chini ya wizara ya usalama wa ndani, ilianzishwa na utawala wa Trump mwaka 2018 baada ya madai kuwa Urusi iliingilia uchaguzi wa mwaka 2016.
Katika misururu ya ujumbe wake katika twitter, Trump alisema kuwa matamshi ya bwana Krebs ya hivi karibuni ya kutetea usalama wa uchaguzi wa Novemba 3 ni maneno yasiyokuwa na ukweli wowote.
Hadi sasa Trump amekataa kukubali ushindi wa Rais mteule wa Marekani Joe Biden na amekuwa mara kwa mara akidai bila ya kuwa na ushahidi kwamba uchaguzi ulikumbwa na udanganyifu na mashini za kupigia kura zilichakachuliwa.
Ghadhabu za kuambiwa ukweli
CISA pamoja na maafisa wa kitaifa wa uchaguzi walitoa taarifa wiki iliyopita iliyosema hapakuwa na ushahidi kwamba uchaguzi ulikuwa na dosari na kusema uchaguzi wa mwaka 2020 ulikuwa moja ya chaguzi zilizokuwa salama katika historia ya chaguzi za Marekani.
Krebs hata hivyo ameonekana kuthibitisha kufutwa kazi na Trump kupitia ujumbe wake wa twitter kwa kusema hivi.
"Nashukuru kuifanyia kazi idara hii, tumefanya kazi kwa usawa, tetea leo ujenge usalama wa kesho."
Kulingana na vyombo vya habari vya Marekani Krebs alijua kuhusu kufukuzwa kwake kazi kupitia ujumbe wa twitter wa Trump. Mark Warner, Naibu mwenyekiti wa kamati ya baraza la seneti inayoshughulikia masuala ya ujasusi amemuunga mkono Krebs baada ya kufutwa kazi.
Warner amesema Krebs ni mfanyakazi bora wa umma na yule ambaye wamarekani wanamhitaji katika masuala ya usalama wa uchaguzi. Amesema inasikitisha kwa rais Trump kumfuta kazi kwa kusema ukweli.
Krebs ni afisa wa pili kufutwa kazi na Donald Trump mwezi huu kupitia twitter. Wiki iliyopita rais huyo alimfuta kazi waziri wa ulinzi Mark Esper.
Rais mteule Joe Biden na makamu wake Kamala Harris bado hawajatoa tamko lolote juu ya kufutwa kazi kwa Chris Krebs.
Mwandishi: Amina Abubakar (AP, Reuters, AFP, dpa)
Mhariri: Josephat Charo