Trump na Xi wakutana Washington
24 Septemba 2026
Ziara hiyo ni ya kwanza kwa Xi nchini Marekani katika kipindi cha karibu miaka mitatu na inakuja wakati Washington na Beijing zikitafuta njia za kudhibiti mvutano uliodumu kwa muda mrefu, hasa katika masuala ya biashara.
Pamoja na tofauti zilizopo, pande zote mbili zinaonyesha nia ya kuendelea na mazungumzo yanayoweza kusaidia kupunguza migogoro ya kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili yenye uchumi mkubwa zaidi duniani.
Waziri wa Fedha wa Marekani, Scott Bessent, amesema Marekanina China zimekubaliana kuongeza muda wa makubaliano ya kusitisha kwa muda mvutano wa kibiashara uliokuwa unatishia kurejesha vita vya ushuru kati ya nchi hizo mbili. Hata hivyo, ubalozi wa China mjini Washington haukutoa tamko la haraka kuhusu kauli hiyo.
Namna Trump alivyomkaribisha Xi Jinping
Mapema kabla ya mazungumzo rasmi, Trump alimkaribisha Xi binafsi katika kituo cha kijeshi cha Joint Base Andrews kilichoko jimboni Maryland. Kitendo hicho kimevutia hisia za wachunguziwa masuala ya diplomasia kwa kuwa ni nadra kwa rais wa Marekani kwenda mwenyewe kumpokea kiongozi wa kigeni katika kituo hicho.
Kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha C-SPAN, mara ya mwisho kwa rais wa Marekani kufanya hivyo ilikuwa mwaka 2015 wakati Rais wa wakati huo, Barack Obama, alipomlaki Papa Francis.
Mkutano huo pia unafanyika wakati Donald Trump akikabiliwa na ukosoaji wa kisiasa nyumbani kuhusu msimamo wake katika mgogoro wa Iran.
Aidha, baadhi ya wabunge wa chama chake cha Republican wameonyesha wasiwasi kuhusu juhudi zake za kuimarisha uhusiano na China, wakidai kuwa Beijing bado ni mshindani mkubwa wa Marekani katika masuala ya usalama na uchumi.
Taiwan yasema inafuatilia kwa karibu mkutano huo
Miongoni mwa masuala nyeti yanayotarajiwa kujadiliwa ni suala la Taiwan. Vyanzo vinavyofahamu maandalizi ya mkutano huo vinasema Xi huenda akasisitiza msimamo wa Beijing kwamba Taiwan ni sehemu ya China. Kwa upande wake, serikali ya Taiwan imesema inafuatilia kwa karibu matokeo ya mazungumzo hayo.
Akizungumza kwa niaba ya Ofisi ya Waziri Mkuu wa Taiwan, msemaji alisema: "Serikali imekuwa ikifuatilia kwa karibu mikutano kati ya viongozi wa Marekani na China. Tunaiona mikutano hiyo kwa mtazamo chanya kwa kuwa inachangia kudumisha utulivu wa kikanda na kupunguza hatari zinazoweza kujitokeza kutokana na upanuzi wa mifumo ya kiimla. Tunaendelea kushirikiana na Marekani katika ngazi zote.”
Xi: Marekani na China ziwe washirika
Mbali na biashara na Taiwan, viongozi hao wanatarajiwa kujadili uwezekano wa kupunguza ushuru katika baadhi ya sekta, kuimarisha ushirikiano dhidi ya biashara ya dawa za kulevya pamoja na kuboresha mawasiliano kati ya majeshi ya nchi hizo mbili.
Xi Jinping amesisitiza kuwa China na Marekani zinapaswa kuwa washirika badala ya mahasimu, akionyesha umuhimu wa ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili katika kipindi ambacho dunia inakabiliwa na changamoto nyingi za kisiasa na kiuchumi.
Ingawa wachambuzi hawatarajii kufikiwa kwa makubaliano makubwa mara moja, mkutano huu unaonekana kuwa hatua muhimu katika kudhibiti mvutano kati ya Washington na Beijing na kuzuia kuzorota zaidi kwa uhusiano wa mataifa hayo mawili makubwa duniani.