1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump amshambulia Harris katika mkutano wa New York

28 Oktoba 2024

Donald Trump amemshutumu Kamala Harris kwa kuiangamiza Marekani, akimshambulia mpinzani wake kwenye mkutano wa hadhara mjini New York. Pia alitoa wito wa hukumu ya kifo kwa mhamiaji yeyote atakayemuua raia wa Marekani.

USA I New York City - Donald Trump spricht im Madison Square Garden
Picha: Andrew Kelly/REUTERS

Mgombea urais wa chama cha Republican Donald Trump alimshambulia Makamu wa Rais Kamala Harris katika mkutano wa hadhara kwenye Ukumbi wa Madison Square, New York, Jumapili usiku. "Umeharibu nchi yetu. Hatutavumilia tena, Kamala, umefukuzwa kazi. Toka kabisa. Umefukuzwa," Trump aliuambia umati. Pia alimwita Harris "mtu mwenye ufahamu mdogo sana."

Soma pia: Wadukuzi wa China wazilenga simu za wagombea urais nchini Marekani

"Uchaguzi huu ni chaguo kati ya kama tutakuwa na miaka minne zaidi ya uzembe na kushindwa, au kama tutaanza miaka bora zaidi katika historia ya nchi yetu," alisema Trump.

Mgombea huyo wa chama cha Republican alitambulishwa na mkewe, Melania Trump, ambaye uwepo wake ulishangaza kwa sababu hajaonekana sana kwenye kampeni zake.

Ukumbi wa Madison Square Garden una nafasi ya watu 20,000Picha: Brendan McDermid/REUTERS

Trump aliahidi nini?

Katika hotuba yake, iliyochukua takriban saa moja na dakika 15, Trump alisisitiza zaidi ahadi alizotoa kwenye kampeni, kama vile kuzuia uhamiaji haramu.

Soma pia: Trump na Harris kuendelea na kampeni za mwisho mwisho

Trump aliendelea kuulaumu uhamiaji haramu kwa kusababisha ghasia za magenge nchini Marekani, akiahidi kuwa atazuia kile alichokiita "uvamizi wa wahalifu wanaoingia nchini humo" ikiwa atashinda uchaguzi wa Novemba 5.

Aidha ametoa wito wa adhabu ya kifo kwa mhamiaji yeyote atakayemuuwa raia wa Marekani au afisa wa polisi. Trump pia aligusia suala la kiuchumi. "Ikiwa nitashinda, tutajenga haraka uchumi mkubwa zaidi katika historia ya dunia. Kitu ambacho tulikuwa nacho katika muhula wetu wa mwisho," Trump alisema.

Harris apiga kampeni Pennsylvania

Je Kamala anaweza kumshinda Trump katika uchaguzi 2024?

01:58

This browser does not support the video element.

Naye Kamala Harris, mwenye umri wa miaka 60, alikuwa na siku yenye shughuli nyingi za kampeni katika jimbo la Pennsylvania ambalo lina umuhimu mkubwa kwenye matokeo ya uchaguzi.

Ziara ya Jumapili ilikuwa safari ya 14 ya makamu huyo wa rais jimboni Pennsylvania tangu alipopata tiketi ya kugombea urais baada ya Rais Joe Biden kujiondoa mwezi Julai. Aliwataka Wamarekani kufanya uamuzi ambao hautawafanya wajutie chochote baada ya siku ya uchaguzi.

Soma pia: Musk atoa zaidi ya dola milioni 44 milioni kumsaidia Trump kwenye kampeni

"Tunaangazia siku zijazo na tunaangazia mahitaji ya watu wa Marekani," Alisema Harris, "kinyume na Donald Trump, ambaye hutumia wakati wote kujitazama kwenye kioo akijiangalia yeye mwenyewe."

Akizungumza mjini Philadelphia, Makamu huyo wa rais aliwataja wapiga kura vijana, akiwasifu kwa "kutaka haraka mabadiliko."

dh/jsi (AP, AFP, Reuters)