1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump amtaka Greta kuziangazia nchi nyingine

22 Januari 2020

Rais wa Marekani, Donald Trump amesema mwanaharakati wa mazingira Greta Thunberg ambaye ni binti mdogo anapaswa kuacha kuinyooshea kidole Marekani na badala yake aziangalie nchi nyingine zinazochafua zaidi mazingira.

UN Greta Thunberg und Donald Trump zufällige Begegnung
Picha: Reuters/A. Hofstetter

 Akizungumza leo na waandishi habari mjini Davos, Uswisi muda mfupi kabla ya kuondoka alikokuwa akihudhuria Kongamano la Kiuchumi Duniani, Trump amesema hadhani kama suala la mabadiliko ya tabia nchi ni la mzaha na angependa kumuona Greta mwenye umri wa miaka 17, akihutubia kwenye jukwaa hilo la kiuchumi. Trump amesema nchi nyingine zimetupa tani kadhaa za uchafu katika Bahari ya Pasifiki na sasa unaelekea Marekani. Amesema Greta anapaswa kulizingatia hilo.

''Nadhani watu wengine wameliweka suala hili katika kiwango ambacho sio cha kweli na kufikia hatua ambayo hatuwezi kuishi maisha yetu. Tunataka kuwa na maji safi zaidi hapa duniani, tunataka kuwa na hewa safi zaidi duniani,'' alifafanua Trump.

Juhudi za kupanda miti 

Trump amesema Marekani itashirikiana na mataifa mengine pamoja na matajiri kuunga mkono juhudi za kupanda miti milioni moja duniani. Mfanyabiashara mkubwa wa Kimarekani, Marc Benioff, amesema dunia inakabiliwa na mzozo wa mabadiliko ya tabia nchi na kwamba miti ni moja ya njia bora za kukabiliana na gesi chafu ya kaboni na kukomesha athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Aidha, Trump amesema hivi karibuni Marekani itaongeza orodha ya nchi ambazo raia wake hawatoruhusiwa kuingia nchini humo. Bado haijawa wazi ni nchi ngapi hasa ambazo zitajumuishwa katika orodha hiyo, lakini Trump amesema kwamba nchi hizo zitatangazwa hivi karibuni, lengo likiwa ni kuilinda Marekani.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen Picha: picture-alliance/dpa/D. Aydemir

Wakati huo huo, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen amezungumzia kuhusu hatari za kiuchumi zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi. Amesema ripoti ya hatari ulimwenguni ya Jukwaa la Kiuchumi Duniani, imebaini kuwa hatari tano za juu za kiuchumi zinahusiana na mabadiliko ya hali ya hewa. Von der Leyen ameahidi kwamba Umoja wa Ulaya utahamasisha Euro trilioni moja za uwekezaji kutoka kwenye vyanzo mbalimbali ili kuanzisha ''uwekezaji wa kimazingira'' ndani ya muongo mmoja.

Rais huyo wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, ameipongeza China kwa kuchukua hatua za kwanza katika juhudi za kuachana na matumizi ya gesi inayochafua mazingira. Amebainisha kuwa tatizo la ongezeko la joto duniani sio tu la nchi moja au chama kimoja au rais mmoja, bali ni la ulimwengu mzima.

(DPA, AFP, Reuters, DW)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW