1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Trump amteua Susie Wiles kuwa Mtendaji Mkuu wa Ikulu

8 Novemba 2024

Rais mteule wa Marekani Donald Trump amemteua Susie Wiles kuwa afisa mkuu wa utumishi wa ikulu ya White House. Huo ni uteuzi wa kwanza wa Trump baada ya ushindi wake kwenye uchaguzi wa Novemba 05 dhidi ya Kamala Harris.

Uchaguzi Marekani 2024 | Susie Wiles
Susie Wiles, mteule kuwa mkuu wa utumishi katika ikulu ya White House katika utawala wa Donald Trump.Picha: Andrew Harnik/AP Photo/picture alliance

Kupitia taarifa, Rais mteule wa Marekani Donald Trump alimteua meneja wake wa kampeni, Susie Wiles, kuwa mkuu wa wafanyakazi wa ikulu ya White House. Huo ukiwa uteuzi wake mkuu wa kwanza tangu kushinda uchaguzi wa wiki hii.

Trump alimmiminia sifa Susie akisema "Susie ni imara, mwerevu, mbunifu, anapendwa na kuheshimiwa kote”. Aliongeza kuwa "Susie ataendelea kufanya kazi bila kuchoka ili Kuifanya Amerika iwe bora zaidi tena. Ni heshima inayostahiki kuwa na Susie kama Mkuu wa kwanza mwanamke wa utumishi wa White House katika historia ya Marekani."

Siku mbili tu baada ya uchaguzi mkuu, na miezi miwili na nusu tu kabla aingie ikulu, ushindi wa kishindo wa Donald Trumpdhidi ya Mdemocrat Kamala Harris tayari unatikisa siasa za Marekani na ulimwengu.

Rais mteule Donald Trump alimshinda Kamala Harris katika uchaguzi wa rais wa Novemba 05, 2024.Picha: Alex Brandon/AP/picture alliance

Trump aashiria nia ya kuzungumza na rais wa Urusi Vladimir Putin

Rais wa Urusi Vladimir Putin, alimpongeza Trump akimtaja kuwa ‘jasiri' kwa jinsi alivyojishughulikia kufuatia jaribio la mauaji katika mkutano wa kisiasa mnamo mwezi Julai, na akasema yuko "tayari" kufanya mazungumzo naye.

"Tabia yake wakati wa jaribio la mauaji ilinivutia. Aligeuka kuwa mtu mwenye ujasiri. Mtu anajidhihirisha katika hali isiyo ya kawaida. Na alijionyesha kwa njia sahihi sana, kwa ujasiri, kama mwanaume, kwa maoni yangu," amesema Putin.

Trump alikiambia kituo cha habari NBC kwamba hajazungumza na Putin tangu alipoibuka mshindi lakini anadhani watazungumza. Viongozi wengi humtizama Putin kuwa kiongozi wa kiimla.

Trump atashughulikiaje mzozo wa Ukraine?

Kauli ya Trump iliashiria mabadiliko makubwa kwa ukimya ambao umekuwepo kati ya rais Jode Biden na Vladimir Putin, tangu Urusi ilipoivamia Ukraine mnamo mwaka 2022, na inatilia maanani ukosoaji wa Trump dhidi ya uungaji mkono wa Marekani kwa Kyiv.

Unaweza kusoma pia Ufuatiliaji wa Afrika katika uchaguzi wa Marekani

Awali rais huyo mteule aliwahi kusema atajaribu mazungumzo ya amani kumaliza mzozo wa Urusi na Ukraine. Lakini rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky aliyezungumza na Trumo siku ya Jumatano alisema miito ya usitishaji mapigano ni hatari.

Rais wa China Xi Jinping alijiunga na viongozi wengine wa ulimwengu kumpongeza Trump, aliyekosolewa na Harris wakati wa kampeni za uchaguzi kwa kuwa na urafiki sana na watawala wa kiimla.

Makamu wa rais Kamala Harris na aliyekuwa mshindani wa Donald Trump, ameahidi kusaidia kwenye mchakato wa makabidhiano madaraka ya amani kwa Trump.Picha: Kevin Lamarque/REUTERS

Trump: Gharama ya fedha haiwezi kuwa kizingiti kuwafurusha wahamiaji wasiokuwa na vibali

Trump alikariri tena mipango yake ya kuwarejesha kwa wingi wahamiaji walioko Marekani bila vibali. Aliliiambia NBC kwamba hana chaguo jingine na kwamba hata gharama ya fedha iwe juu kiasi gani, atahakikisha hilo limetekelezwa.

Huku Trump akianza kuweka mipango yake ya kupokea Madaraka, Rais Biden ameahidi makabidhiano ya amani ya Madaraka.

Biden, mwenye umri wa miaka 81, aliwasihi Wamarekani katika hotuba yake ya televisheni "kupunguza joto la kisiasa," hali ambayo ni kinyume kabisa na uchaguzi wa mwaka 2020 wakati Donald Trump alipokataa kukubali kushindwa.

(Chanzo: AFPE)