Trump anaashiria ushindi wa mapambano dhidi ya IS
7 Februari 2019Rais Donald Trump amewaambia wawakilishi wa muungano wa mataifa 79 yanayoongozwa na Marekani katika mapambano dhidi ya wafuasi wa itikadi kali wa Dola la Kiislam au Daesh kwamba wanamgambo hao wanadhibiti sehemu ndogo tu ya ardhi wanayodai kuwa ni ya utawala wao au Khalifa:"Wanajeshi wa Marekani, washirika wetu na vikosi vya kidemokrasi nchini Syria wameikomboa takriban ardhi yote iliyokuwa hapo awali ikidhibitiwa na IS nchini Syria na Iraq. Kimsingi habari hizo huenda zikatangazwa wakati wowote kutoka sasa, pengine wiki inayokuja, kwamba tunadhibiti asili mia kwa mia ya ardhi au Khalifat. Lakini nataka kusubiri hadi tamko rasmi . Sitaki kulisema kabla."
Marekani inashikilia mpango wa kuwarejesha nyumbani wanajeshi
Maafisa wa Marekani walisema IS wamepoteza asili mia 99.5 ya ardhi yao na kwamba wanadhibiti chini ya kilomita za mraba 5 nchini Syria, katika vijiji vya bonde la mto Euphrates.
Hata hivyo kuna hofu, uamuzi wa kuondolewa wanajeshi wa Marekani usije ukavuruga matumaini hayo. Rais Trump amewaambia washirika katika mapambano dhidi ya IS waliokutana katika wizara ya mambo ya nchi za nje kwamba ingawa "idadi ndogo ya waliosalia kutoka kundi hilo bado ni hatari" hata hivyo ameamua kuwarejesha nyumbani wanajeshi wa Marekani. Amewatolea wito washirika wasimame kidete na kuchangia ipasavyo katika mapambano dhidi ya ugaidi.
Wanamgambo wasiopungua 5000 wa IS wamejificha Syria
Hata baada ya rais Trump na waziri wake wa mambo ya nchi za nje Mike Pompeo kutetea umuhimu wa kuwarejesha nyumbani wanajeshi wa Marekani, uamuzi uliowashitua washirika wao na kupelekea waziri wa ulinzi Jim Mattis kujiuzulu baadhi ya wakuu wa kijeshi bado wana wasi wasi.
Wanaharakati wanaofuatilia kwa makini mzozo nchini Syria wanazungumzia dalili za kuongezeka uasi. Rami Abdulrrahman anaeongoza shirika lenye makao yake nchini Uingereza la kusimamia masuala ya haki za binaadam nchini Syria anasema IS bado wana wapiganaji kati ya 4000 hadi 5000 na wengi wamejificha misituni na milimani.
Umoja wa Mataifa pia umechapisha ripoti inayowataja IS kuwa "kitisho kikubwa cha magaidi ulimwenguni."
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AP
Mhariri: Iddi Ssessanga