Trump anatathmini pendekezo jipya la Tehran kwa mashaka
3 Mei 2026
Rais wa Marekani Donald Trump alisema siku ya Jumamosi kwamba alikuwa anapitia pendekezo jipya la Iran la kumaliza vita. "Nitawaambia baadaye," aliwaambia waandishi wa habari, akiongeza kuwa "watanipa majibu kamili sasa hivi."
Muda mfupi baadaye, Trump aliandika kwenye mtandao wake wa Truth Social kwamba "hafikiri kuwa pendekezo hilo linaweza kukubalika kwa sababu bado Iran haijalipa gharama kubwa ya kutosha kwa yale iliyoyafanya kwa ubinadamu na dunia kwa miaka 47 iliyopita."
Kauli ya Trump ilikuja baada ya kukataa pendekezo la awali la Iran mapema wiki hii.
Iran ilisema Jumamosi kwamba ni juu ya utawala wa Trump kuamua kama utafuata suluhisho la mazungumzo au kurejea katika vita vya wazi.
"Sasa mpira uko mikononi mwa Marekani kuchagua njia ya diplomasia au kuendelea na makabiliano", Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Kazem Gharibabadi aliwaambia wanadiplomasia mjini Tehran, kulingana na kituo cha taifa cha IRIB.
"Iran, kwa lengo la kulinda maslahi na usalama wake wa kitaifa, iko tayari kwa njia zote mbili," alisema.
Wakati huo huo, Mohammad Jafar Asadi, kiongozi wa juu katika kamandi ya kati ya jeshi la Iran, alisema "uwezekano wa mzozo mpya kati ya Iran na Marekani upo."
"Ushahidi umeonyesha kwamba Marekani haizingatii ahadi au makubaliano yoyote," shirika la habari la Fars lilimnukuu akisema.
Israel yashambulia baadhi ya maeneo ya kusini mwa Lebanon
Jeshi la Israel lilifanya mashambulizi kusini mwa Lebanon siku ya Jumamosi, na kuua watu kadhaa, kulingana na shirika la habari la serikali ya Lebanon. Jeshi la Israel lilisema lilishambulia malengo kadhaa ya Hezbollah.
Mashambulizi hayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara licha ya kuwepo kwa makubaliano dhaifu ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hezbollah. Maandishi ya makubaliano hayo yanaruhusu Israel kuchukua hatua dhidi ya kile kinachokiita "mashambulizi yaliyopangwa, ya karibu au yanayoendelea."
Pande zote mbili zimekuwa zikishutumiana kwa kukiuka makubaliano hayo. Hezbollah nayo ilidai kufanya mashambulizi kadhaa dhidi ya wanajeshi wa Israel.
Kundi hilo la wanamgambo wa Kishia liliingiza Lebanon katika vita vya Mashariki ya Kati tarehe 2 Machi kwa kuunga mkono mfadhili wake Iran. Tangu wakati huo, mashambulizi ya Israel yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 2,600 nchini Lebanon na kusababisha zaidi ya milioni moja kuyahama makazi yao.
Wakaazi watakiwa kuondoka
Jeshi la Israel pia liliwaonya wakazi wa miji na vijiji kadhaa kusini mwa Lebanon kuhama makazi yao huku likijiandaa kufanya mashambulizi mapya, licha ya kuwepo kwa usitishaji mapigano kati ya nchi hizo mbili.
Jeshi hilo lilisema linaendesha operesheni dhidi ya Hezbollah inayoungwa mkono na Iran, ambayo linadai inakiuka makubaliano ya kusitisha mapigano.
"Kwa usalama wenu, lazima muondoke mara moja majumbani mwenu na mjiondoe angalau mita 1,000 kuelekea maeneo ya wazi," msemaji wa jeshi kwa lugha ya Kiarabu, Avichay Adraee, aliandika kwenye mtandao wa X.
Tahadhari hiyo ilihusu vijiji na miji 11, ikiwa ni pamoja na baadhi katika wilaya ya Nabatieh, kaskazini mwa Mto Litani. Wanajeshi wa Israel wanadhibiti ukanda wa kusini mwa Lebanon, kusini mwa mto huo.
Vyombo vya habari vya Lebanon baadaye viliripoti mashambulizi ya Israel katika maeneo mbalimbali kusini mwa Lebanon, ikiwemo miji ambayo haikuwa imeonywa kuhama.