1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump aongoza kinyang'anyiro cha kuwania urais

17 Januari 2024

Donald Trump ameshinda kwenye kinyang'anyiro cha kwanza cha kuwania uteuzi wa kugombea urais wa Marekani kupitia Republican akithibitisha jinsi alivyo na nguvu licha ya kukabiliwa na mkururo wa kesi mahakamani.

Donald Trump akiwashukuru wapigakura wa Iowa kwa kumpa ushindi kwenye kura za mchujo.
Donald Trump akiwashukuru wapigakura wa Iowa kwa kumpa ushindi kwenye kura za mchujo.Picha: Andrew Harnik/AP/picture alliance

"Hili ni tukio la fahari kubwa. Hii  ni mara ya tatu kwa sisi kushinda. Lakini huu ni ushindi mkubwa kabisa. Walisema ukishinda kwa asilimia 12 ni ushindi mkubwa. Hilo litakuwa jambo gumu kulifikia. Lakini nadhani tumepindukia mara mbili. Nakisia hata pengine imepindukia mara tatu." Alisema Trump usiku wa Jumatatu (Januari 15) wakati akiwashukuru wapigakura wa chama chake kwenye uchaguzi huo uliofanyika katika jimbo la Iowa.

Bilionea huyo mwenye umri wa miaka 77 alipata asilimia 51 ya kura, akifuatiwa na Gavana wa Florida, Ron DeSantis, aliyepata asilimia 21 na balozi wa zamani wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Nikki Haley, aliyepata asilimia 19. 

Soma zaidi: Warepublican wa jimbo la Iowa, Marekani kuamua mgombea urais

Huu unatajwa kuwa ushindi mkubwa zaidi kuwahi kupatikana kwa mtia nia ya kuwania urais kupitia Republican, tangu ule wa Bob Dole aliyeshinda kwa tafauti ya asilimia 12.8 mwaka 1988.

Ushindi wa Trump kwenye jimbo hilo unaonesha kutokuyumba kwa wafuasi wake hata baada ya uvamizi wa tarehe 6 Januari 2021 dhidi ya jengo la bunge, Capitol Hill, na mashitaka 91 ya uhalifu dhidi yake kwa kujaribu kuyapinduwa matokeo ya uchaguzi wa 2020, kukutwa na nyaraka za siri baada ya kuondoka madarakani na kughushi taarifa za malipo ya fedha kwa muigizaji mmoja wa sinema za uchafu.

Trump ametumia matatizo yake hayo ya kisheria kuchangisha fedha na kuongeza ufuasi wake, akijenga hoja kwamba yeye hana makosa bali amefanywa tu kuwa mbuzi wa kafara katika mchezo wa kumsaka mchawi.

Zaidi ya nusu wa Warepublican wamuunga mkono Trump

Uchunguzi wa maoni unaonesha kuwa zaidi ya nusu ya wapigakura wa Republican wanayaamini madai ya uongo ya Trump kwamba ushindi wake kwenye uchaguzi wa mwaka 2020 uliibiwa, wakisema hawadhani ikiwa kweli Joe Biden alimshinda kihalali Trump.

Gavana Ron DeSantis wa Florida aliyeshika nafasi ya pili kwenye kura za mchujo za Iowa.Picha: Christian Monterrosa/AFP/Getty Images

Zaidi ya asilimia 60 wanasema kuwa bado Trump anafaa kuwa rais hata kama atatiwa hatiani kwa uhalifu anaoshitakiwa nao. 

Soma zaidi: Biden aonya juu ya urais wa Donald Trump wakati wa kukumbuka uvamizi wa jengo la Bunge, Januari 6, 2021

Kihistoria, jimbo la Iowa limekuwa likichukuliwa kama kigezo cha mwenendo cha uchaguzi kutokana na kuwa kwake la awali kwenye kalenda ya kampeni, lakini si kila mara mshindi wa jimbo hilo humalizikia kuwa mgombea urais, kama ilivyotokea mwaka 2008, 2012 na 2016.

Lakini Trump anataka kuuharakisha mchakato huo, ambao kwa kawaida unachukuwa miezi kadhaa, kwa kuhakikisha kuwa anapata ushindi mkubwa kwenye chaguzi za awali ili kuwalazimisha washindani wake kujiondowa na mapema.

Wa kwanza kufanya hivyo alikuwa Vivek Ramaswamy, ambaye baada ya kupata asilimia nane tu ya kura hapo hapo jana, alitangaza kujitowa kwenye kinyang'anyiro hicho na badala yake akawataka wafuasi wake kumuunga mkono Trump.

Vyanzo: Reuters, AFP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW