1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump ajitokeza mkutano wa RNC baada ya shambulio

16 Julai 2024

Donald Trump amepokea makaribisho ya kishujaa alipojitokeza kwenye mkutano mkuu wa chama cha Republican pamoja na mgombea mwenza wake JD Vance -- mara ya kwanza kuonekana hadharani tangu jaribio la mauaji dhidi yake.

USA | Milwaukee, Wisconsin | Mkutano Mkuu wa Republican | Trump
Trump alipoekelewa kwa vishindo na wajumbe wa mkutano mkuu wa chama cha Repblican, RNC, baada ya kumpitisha rasmi kuwa mgombea wao katika uchaguzi mkuu wa Novemba 5.Picha: Angela Weiss/AFP via Getty Images

Saa chache baada ya kushinda uteuzi rasmi wa kuwa mgombea urais wa Republican na kumtangaza Seneta wa mrengo wa kulia J.D. Vance kuwa mgombea mwenza wake, Trump aliingia kwenye ukumbi wa mkutano huo mkuu mjini Milwaukee akiwa amefungwa bendeji kwenye sikio lake la kulia.

Lilikuwa tukio la pili kubwa siku hiyo kwa umati wa chama cha Republican, ambao ulilipuka kwa shangwe mapema wakati Trump alipomtangaza Vance, mwenye umri wa miaka 39 kuwa makamu wake wa rais, akimtuza mkosoaji waka mkali zaidi wa wakati mmoja ambaye amekuwa mmoja wa wafuasi wake wakereketwa.

Soma pia: Trump amchagua Seneta JD Vance kama mgombea mwenza

Wakati Trump, mwenye umri wa miaka 78, anazidi kujiamini kurejea Ikulu ya White House, licha ya matatizo mengi ya kisheria na majaribio mawili ya kumuondoa madarakani yaliougubika muhula wake wa kwanza, mpinzani wake Rais Joe Biden anakabiliwa na kuporomoka kwa umamarufu wake miongoni mwa wapigakura na wasiwasi ndani ya chama chake cha Democratic kuhusu hali yake ya kiafya.

Mgombea wa nafasi ya makamu wa rais wa Republican J.D. Vanace akisalimiwa na wafuasi wakati akiwasili kwa mkutano wa kwanza wa taifa wa RNC mjini Milwauke, Wisconsin, Julai 15, 2024.Picha: Mike Segar/REUTERS

Makamu wa rais mwenye uzoefu mdogo zaidi?

Chaguo la Trump la makamu wa rais, Vance, ni mmoja wa wateule walio na uzoefu mdogo zaidi wa nafasi ya makamu wa rais katika historia ya sasa ya Marekani, lakini anaunga mkono sera kali za rais huyo wa zamani, zikiwemo za kupinga uhamiaji na kutanguliza maslahi ya Marekani, na msimamo wake ni mkali kuliko hata wa Trump kwenye baadhi ya masuala, kama vile utoaji mimba.

Vance alizungumza na kituo cha televisheni cha Fox, siku ya Jumatatu, ambapo alielezea makubaliano yake na Trump kuhusu sera ya kigeni na kuukosoa utawala wa Rais Joe Biden. Vance alisifu namna Trump alivyoshughuliki kundi linalojiita Dola la Kiislamu akiwa madarakani na kuzielezea sera za Biden kuelekea Iran kuwa zisizo na ufanisi.

Soma pia: Viongozi mbalimbali walaani jaribio la mauaji dhidi ya Trump

Pia alikosoa jinsi rais alivyoshughulikia vita vya Israel na Hamas na sera yake ya Ukraine.

"Urusi isingeivamia Ukraine kama Donald Trump angekuwa rais. Kila mtu anakubaliana nayo. Hata wenzangu wengi wa Democratic wanakubaliana na hilo kwa siri. Sasa tumetumia dola bilioni 200. Lengo ni nini? Je, tunajaribu kutimiza nini?", alihoji Vance.

"Rais Trump ameahidi kujadiliana na Urusi na Ukraine na kumaliza hili ili tujikite kwenye suala halisi, ambalo ni China."

Trump aliliambia gazeti la New York Post kuwa alikuwa ameandaa hotuba kali kuhusu utawala mbovu wa Biden, na baadhi ya Warepublican walitaka kulaumu matamshi ya Wademocrat kwa shambulio dhidi ya Trump, lakini sasa amefuta hotuba hiyo na kuandaa nyingine ambayo anatumai itaiunganisha nchi.

Biden azidi kupongezwa kwa ushindi licha ya Trump kukataa kukubali kushindwa

01:06

This browser does not support the video element.

Nini cha kutarajia siku ya pili ya mkutano?

Wazungumzaji kwenye siku ya pili ya mkutano huo wanatarajiwa kutaja kile Warepublixan wengi wameelezea kama nguvu na uthabiti wa rais huyo wa zamani baada ya tukio la kushambuliwa mjini Pennsylvania.

Hotuba nyingi zinatazamiwa kujikita juu ya uhamiaji, kaulimbiu ikiwa "Tuifanye Amerika kuwa salama kwa mara nyingine tena."

Soma pia: Biden asema hang'oki licha ya makosa ya aibu

Nikki Haley huenda akawa mmoja wa wazungumzaji wa siku ya pili. Balozi huyo wa zamani wa Umoja wa Mataifa na gavana wa jimbo la South Carolina alikuwa mpinzani mkuu wa mwisho dhidi ya Trump katika kinyang'anyiro cha mchujo.

Wiki iliyopita, alitangaza kwamba angewaagiza wajumbe wake wa mkutano kumpigia kura Trump, lakini akasema kwamba hatahudhuria kongamano hilo. Lakini ofisi yake ilisema baada ya tukio la Trump kupigwa risasi kwamba angezungumza kwenye mkutano huo.