1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump arudi kortini mkesha wa ushindi New Hampshire

22 Januari 2024

Donald Trump amerejea Jumatatu kwenye kesi yake ya kashfa ya unyanyasaji wa kijinsia New York katika mkesha wa kura ya mchujo ya New Hampshire ambapo anatazamiwa kumshinda mpinzani wa mwisho aliyesalia, Nikki Haley.

Marekani | Donald Trump na Ron DeSantis
Kicha ya kukabiliwa na kesi lukuki, Donadl Trump, kulia, anaonekana kuwa njiani kushinda uteuzi wa chama cha Republican kugombea dhidi ya Rais Joe Biden.Picha: Richard Graulich/The Palm Beach Post via ZUMA Wire/picture alliance

Uchaguzi wa mchujo unaonekana kuwa nafasi ya mwisho na bora zaidi kwa Nikki Haley kumzuia Trump, ambaye licha ya kupigiwa kura mara mbili ya kumuvua madaraka kama rais na sasa anakabiliwa na kesi nne za jinai, amefaulu kuweka chapa yake ya mrengo mkali wa kulia kwa chama kizima cha Republican.

Kura mpya ya maoni ya Washington Post/Monmouth Jumatatu ilionyesha Trump, 77, akiungwa mkono na asilimia 52 New Hampshire dhidi ya asilimia 34 ya Haley.

Haley, gavana wa zamani wa jimbo la South Carolina, sasa ndiye mpinzani pekee baada ya Gavana wa Florida Ron DeSantis kujiondoa mwishoni mwa juma.

Lakini atahjitaji muujiza wa kisiasa kuweza kumzuwia Trump, ambaye anaonekana kurudia ubabe wake katika kinyang'anyiro cha kwanza jimboni Iowa, na kisha ashinde chaguzi zilizosalia za mchujo ili kuwa mteule wa kuchuana na Rais Joe Biden mnamo Novemba.

Soma pia: Trump akaribia uteuzi wa chama chake huko New Hampshire

Badala ya kuficha matatizo yake mengi ya kisheria, Trump amegeuza vikao vya mahakama kuwa matukio ya kampeini, akidai kwamba kila kesi ni sehemu ya jaribio la chama cha Democratic kumzuia kurejea White House kwa muhula wa pili.

Donald Trump akiwa na gavana wa Florida Ron DeSantis, kulia, ambaye amejitoa kwenye kinyang'anyiro cha kuwa uteuzi wa chama cha Republican na kumuidhinisha Trump.Picha: Joe Burbank/Orlando Sentinel via ZUMA Press/picture alliance

Ujumbe huo unaweza kuwavutia tu wafuasi wa mrengo mkali wa kulia wa Republican lakini wao ndio msingi wa kushinda uteuzi wa Republican. Siku ya Jumatatu, Trump alichagua kurudia mtindo huu, akipanga kuhudhuria kesi yake ya udhalilishaji wa kiraia mjini New York na kurudi New Hampshire pekee kwa ajili ya mkutano wa usiku wa kupiga kura.

E. Jean Carroll, mwandishi mwenye mafanikio, anataka fidia ya zaidi ya dola milioni 10 kwa kukashifiwa na Trump, ambaye mahakama nyingine ya kiraia ya New York ilimpata na hatua ya udhalilishji wa kingono dhidi yake.

Trump anakabiliwa na kesi nyingine kubwa za uhalifu, ikiwa ni pamoja na jaribio lake la kupindua matokeo ya uchaguzi wa 2020 ambapo alishindwa na Biden.

Nikki Haley amgeukia bosi wake wa zamani

Haley, ambaye aliwahi kuwa balozi wa Umoja wa Mataifa chini ya Trump, amemgeukia vikali bosi wake wa zamanii katika siku chache zilizopita, akigusia mfululizo wa kujikwaa na makosa wakati wa hotuba zake kama ishara kwamba anapoteza uwezo wake wa kiakili.

"Hayuko katika kiwango sawa alichokuwa nacho mwaka 2016. Nadhani tunashuhudia baadhi ya kupungua huko. Lakini zaidi ya hayo, nitakachosema ni kujikita kwenye ukweli ambao bila kujali nini, vurugu zinamfuata," aliiambia CBS.

Pia anatumai kunufaika na idadi kubwa ya wapiga kura wasioegemea upande wowote huko New Hampshire, badala ya wapigakura wa Republican wenye msimamo mkali zaidi wa Iowa.

Lakini baada ya DeSantis kujiondoa kwenye kinyang'anyiro na kumuidhinisha Trump, mfanyabiashara huyo aliyekumbwa na kashfa na rais wa zamani anaonekana kuwa ngumu kuzuwiwa.

Balozi wa zamani wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley ndiye mgombea aliesalia kupambana na bosi wake wa zamani. Picha: Robert F. Bukaty/AP Photo/picture alliance

Trump alimtaja Haley kama "mtu wa kimataifa" mwishoni mwa juma -- kauli ya kejeli kwa mtu anayejitenga, mzalendo wa mrengo wa kulia ambavyo amehimiza wakati wa kupanda kwake kileleni mwa siasa za Republican.

Soma pia: Trump apigwa marufuku kushiriki uchaguzi wa mchujo katika jimbo la Maine

Tofauti na hoja ya Trump akiwa rais na sasa kama mgombea kwamba Marekani inapaswa kuzingatia upya ushirikiano wa kihistoria na hata uanachama wa NATO, Haley anapendekeza sera ya kigeni ya jadi, na isiyo ya amani ya Republican.

Iwapo Haley atafanya vyema siku ya Jumanne, hiyo inaweza kumfanya apate msisimko kwa wakati kwa ajili ya mchujo unaofuata katika jimbo lao la South Carolina mwishoni mwa Februari.

Hata hivyo kufikia wakati huo, Trump anaweza kuwa njiani kuelekea kitu kama kutawazwa, kwenye kile kichachoitwa "Super Tuesday" mnamo Machi 5, wakati ambapo wajumbe 874 watakapopiga kura inayoweza kumpa mgombea robo tatu ya kura jumla zinazohitajika kwa uteuzi.

Wasaidizi wanatarajia Trump kuwa katika nafasi ya kufunga kinyang'anyiro wiki moja baadaye na wanataka wawe wamekamilisha kazi ifikapo Aprili -- karibu kabla ya kuanza kwa kesi yoyote ya uhalifu dhidi yake.

Chanzo: AFP