Trump arudisha nyuma baadhi ya sera za Obama kwa Cuba
17 Juni 2017Wakati wahafidhina wanaompinga Castro wamekaribisha hatua za kurudisha nyuma baadhi ya sera za maridhiano za aliyekuwa rais Barack Obama na Cuba wabunge kadhaa wa chama cha Republikan hususan kutoka majimbo ya kilimo wamekosowa mabadiliko hayo kuwa ni potofu na ya kujitenga.Wamemtaka rais aregeze vizingiti kati ya nchi hiyo na Cuba ili kukuza biashara na kuzalisha ajira kwa nchi zote mbili.
Mbunge wa chama hicho Rick Crawford wa jimbo la R-Ark amesema mabadiliko hayo ya Trump yatakuwa na madhara zaidi mbali na kuppoteza fursa kwa eneo la vijiji la Marekani ambalo lingefaidika na kwa kupata nafasi kubwa zaidi ya kuingiza bidhaa katika soko la kilimo la Cuba.
Amesema sera ya Trump yumkini ikauweka hatarini usalama wa taifa wakati washindani muhimu wakichukuwa hatua ya kuziba pengo hilo.
Crawford ameongeza kusema kutojihusisha huko zaidi kwa Marekani kunafunguwa fursa kwa nchi nyengine kama vile Iran,Urusi,Korea Kaskazini na China kujipatia ushawishi kwa kisiwa hicho kilioko maili 90 nje ya mwambao wa Marekani.
Maslahi kwa nchi zote mbili
Naye seneta Jeff Flake wa R-Ariz ambae alikuwa akimkosowa Trump mara kwa mara wakati wa kampeni za urais mwaka 2016 amesema katika taarifa kwamba sera yoyote ile ambayo inapunguza uwezo wa Wamarekani kusafiri huru kwenda Cuba haina maslahi kwa Marekani au kwa wananchi wa Cuba.
Flake alikuwa miongoni mwa wabunge wakosoaji wakubwa kabisa wanaopinga kurudishwa nyuma kwa hatua za Obama kupatana na Cuba.Ameonya kwamba kurudi katika sera za kuiwekea ngumu Cuba kunamuumiza kila Mcuba ambaye maisha yake yanazidi kutegemea shughuli za usafiri na utalii.
Katika taarifa yake Flake ametowa wito kwa uongozi wa kamati ya seneti kuruhusu muswada huo kupigiwa kura ambao amesema utaondowa taratibu za vurugu kwa safari za kwenda Cuba ambazo haziko kwa safari za Wamarekani kwenda katika nchi yoyote ile duniani.Muswada huo una wadhamini wenza 54 wakiwemo wabunge tisa wa Republikan.
Cuba yashutumu Marekani
Cuba hapo Ijumaa imeshutumu hatua ya Rais Doland Trump kurudisha nyuma kile alichokiita "makubaliano ya upande mmoja kabisa ya utawala wa Obama na Cuba."
Serikali imesema katika taarifa yake kupitia televisheni ya taifa kwamba inashutumu hatua hizo mpya za kuimarisha vikwazo ambazo zitashindwa.Hata hivyo serikali hiyo ya Cuba pia imesisitiza kuwa tayari kwake kuendelea na mazungumzo ya heshima na ushirikiano kwa masuala ya maslahi ya nchi hizo mbili.
Mapema hapo Ijumaa Trump amesema anafuta makubaliano ya mtangulizi wake Barack Obama na kisiwa hicho cha Kikoministi ambacho kimerudisha uhusiano wa kibalozi baada ya miaka hamsini.
Trump amewaambia Wamarekani wenye asili ya Cuba huko Miami kwamba atabana baadhi ya vikwazo vya safari na biashara na Cuba juu ya kwamba ameziachilia bila ya kuzigusa hatua za mageuzi mbali mbali yalioachwa na Obama.
Trump ametowa wito wa kufanyika mbadiliko nchini Cuba ikiwa ni pamoja na kuachiliwa huru kwa wafungwa wa kisiasa,kuitisha uchaguzi huru na wa haki na kuheshimu uhuru wa kuzungumza na wa kukusanyika.
Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/dpa
Mhariri: Yusra Buwayhid