Trump afuta awamu ya pili ya mashambulizi Venezuela
9 Januari 2026
Rais huyo wa Marekani pia amesifia ushirikiano chanya kati ya mataifa hayo mawili, hasa katika miundombinu ya mafuta na gesi, baada ya wiki iliyopita, Marekani kumvamia na kumkamata rais wa Venezuela Nicolas Maduro na mkewe Cilia Flores. Hii ni baada ya miezi kadhaa ya Marekani kuukashifu utawala wa Maduro.
"Kwa sababu ya ushirikiano huu, nimefutilia mbali uvamizi wa pili dhidi ya Venezuela. Sidhani kama hilo linahitajika. Lakini meli zote zitaendelea kuwepo pale pale kwaajili ya ulinzi na usalama," aliandika Trump katika mtandao wake wa Truth Social, akimaanisha meli za kivita za Marekani zilizopo pwani ya Venezuela.
Trump aliendelea kuandika kuwa, Venezuela kuwaachiwa wafungwa wa kisiasa ni ishara ya kusaka amani. Serikali mjini Caracas awali ilitangaza kuwaachia wafungwa hao wa kisiasa na wale wa kigeni akiwemo mwanasiasa mashuhuri wa upinzani kama mwanaharakati wa kutetea haki za binaadamu Rocío San Miguel. Waandishi habari waliokamatwa pia waliachiwa.
Marekani imesema hatua ya Venezuela imekuja kufuatia ombi lake. Wengine walioachiwa ni pamoja na Enrique Marquez, aliyekuwa mpinzani wa maduro katika Uchaguzi Mkuu wa 2024 na kiongozi wa upinzani Biagio Pilieri, aliyesimamia kampeni ya urais ya mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Maria Corina Machado mwaka uo huo. Lakini idadi hasa ya wafungwa walioachiwa bado haijajulikana.
Machado kukutana na Trump
Katika mahojiano yake aliyoyafanya na shirika la habari la Fox, Trump alisema anatarajia kukutana na Machado wiki ijayo mjini Washington. Baada ya kumkamata Maduro Trump alisema Machado hana uungaji mkono wa watu wa Venezuela wala heshima ya raia hao ya kumuezesha kuliongoza taifa hilo.
Licha ya maneno hayo, bado Maria Machado alimpongeza kwa kile alichokifanya Venezuela, akisema ni hatua ya kihistoria na kubwa ya kueleka mabadilishano ya kidemokrasia. Mchado alikabidhiwa tuzo ya amani ya Nobel mwaka uliopita, tuzo ambayo Trump aliitaka kwa udi na uvumba.
Kampuni za mafuta kuwekeza Venezuela
Trump anataka uwekezaji mkubwa wa mafuta. Kulingana na rais huyo wa Marekani, kampuni kubwa za mafuta Marekani zinatarajiwa kuwekeza dola bilioni 100 nchini Venezuela.
Mkutano na viongozi wa kampuni hizo unatarjiwa kufanyika katika Ikulu ya White House leo Ijumaa (09.01.2025). Trump amesema miundombinu ya mafuta na gesi Venezuela inapaswa kujengwa upya katika mfumo ulio bora, mkubwa na wa kisasa.
Wiki iliyopita wanajeshi wa Marekani walimkamata Maduro na mkewe mjini Caracas na kuwasafirisha hadi Marekani ambako wanashitakiwa kwa makosa yanayohusiana na ulanguzi wa madawa ya kulevya. Mrithi wake, Delcy Rodríguez, ambae ni mfuasi mkubwa wa Maduro, amekosoa kukamatwa kwake akisema ni ukiukwaji wa haki za kimataifa.