1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump: Bin Salman hajui lolote kuhusu mauwaji ya Khashoggi

19 Novemba 2025

Rais wa Marekani Donald Trump alimtetea Mwana Mfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman kuhusu mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi mwaka 2018.

Marekani Washington D.C. 2025 | Mkutano kati ya Donald Trump na Mohammed bin Salman katika Ikulu ya White House
Rais Donald Trump na Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman wafanya mkutano wa pande mbili katika Ofisi ya Oval katika Ikulu ya White House huko Washington DC Jumanne, Novemba 18, 2025Picha: Nathan Howard/UPI Photo/Newscom/picture alliance

Katika kauli hiyo Trump alisisitiza kuwa mtawala huyo wa kifalme "hakujua chochote” kuhusu mauaji hayo huku akimkaribisha kwa heshima Ikulu ya White House.

Marekani na Saudi Arabia ziliidhinisha makubaliano ya nyuklia kwa matumizi ya kiraia na mauzo ya ndege za kivita aina ya F-35, huku Trump akijaribu kufunika suala la mauaji ya mwandishi wa gazeti la Washington Post.

Swali lililomkasirisha Rais Trump

Trump alikasirika kwa mwandishi wa habari aliyemuuliza Mwanamfalme kuhusu mauaji hayo akisema swali hilo "linamvunjia heshima” mgeni wake katika ziara yake ya kwanza Marekani tangu mauaji hayo, na kumuita Khashoggi "mtu mwenye utata mkubwa.”

Kauli ya Trump inapingana na tathmini ya kijasusi ya Marekani ya mwaka 2021 iliyohitimisha kuwa Mwana Mfalme Mohammed aliagiza operesheni ya kumuua Khashoggi, ambaye aliuawa ndani ya ubalozi wa Saudi Arabia mjini Istanbul.

Kadhalika mwana mfalme wa Saudi Arabia, aliyewasili nchini Marekani na ahadi ya uwekezaji wa dola trilioni moja nchini Marekani katika ziara yake ya kwanza tangu mauaji, alisema mauaji ya Khashoggi yalikuwa "ya kuumiza” na "makosa makubwa.

Mazungumzo Kuhusu Uhusiano na Israel

Aidha katika mazungumi hayo Trump alisema amepata "majibu chanya” kuhusu uwezekano wa Saudi Arabia kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel.  "Nadhani tuko vizuri, unajua, sitaki kutumia neno ‘ahadi', lakini tumekuwa na mazungumzo mazuri sana kuhusu Mikataba ya Abraham. Tumeeleza kuhusu suluhisho la taifa moja, mataifa mawili. Unajua, tumegusia mambo mengi kwa muda mfupi. Tutayajadili zaidi pia. Lakini nadhani una mtazamo mzuri sana kuhusu Mikataba ya Abraham."

Rais Donald Trump na Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman wafanya mkutano wa pande mbili katika Ofisi ya Oval katika Ikulu ya White House huko Washington DC Jumanne, Novemba 18, 2025Picha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

Lakini mwana mfalme alifafanua kuwa ingawa anataka kujiunga na Mkataba wa Abraham, anashikilia sharti lake kwamba Israel lazima itoe njia ya kuanzisha taifa la Palestina, jambo ambalo Israel imekataa kufanya."Tunaamini. Tunaamini kuwa  na uhusiano mzuri na nchi hizi mbalimbali ni jambo jema. Na tunataka kuwa sehemu ya Mkataba wa Abraham, lakini pia tunataka kuhakikisha kuwa tunapata njia iliyo wazi ya suluhisho la mataifa mawili. Na leo tumekuwa na mazungumzo mazuri na Mheshimiwa Rais kwamba tutafanya kazi juu ya hilo ili kuhakikisha tunaandaa mazingira sahihi haraka iwezekanavyo ili hilo lifanikishwe."

Heshima ya Kifalme na changamoto za makubaliano ya nyuklia

Awali, Trump alimkaribisha bin Salman kwa tabasamu na mkono wa salamu kwenye zulia jekundu, huku makumi ya wanajeshi wakipanga mstari kuzunguka eneo hilo. Limousine iliingizwa kwenye Ikulu ikisindikizwa na kikosi cha heshima cha Jeshi la Marekani cha wapanda farasi. Viongozi hao wawili kisha walitazama angani wakati ndege za kivita zikapita kwa kishindo.

Bin Salman na ujumbe wake walikula chakula cha mchana na Trump pamoja na wasaidizi wake katika Chumba cha Baraza la Mawaziri na alitarajiwa kuhudhuria chakula cha jioni cha heshima chenye vazi rasmi lililofahamika kuwa black-tie Ikulu ya White House, jambo lililompa sura ya ziara ya kitaifa.

Bin Salman amekuwa akitafuta makubaliano kama hayo ili kufungua njia ya kupata teknolojia ya nyuklia ya Marekani na kusaidia Saudi Arabia kufikia kiwango cha Umoja wa Falme za Kiarabu na adui wake wa jadi, Iran.

Lakini maendeleo ya makubaliano ya nyuklia yamekuwa magumu kwa sababu Wasaudi wamekataa sharti la Marekani linalopiga marufuku kurutubisha urani au kuchakata tena mafuta yaliyotumika njia zote mbili zinazoweza kuelekea kutengeneza bomu.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW