Trump asema Marekani imeimarika zaidi
25 Februari 2026
Hotuba hiyo imepewa uzito mkubwa na vyombo vya habari sio tu ndani ya Marekani bali kimataifa kwa sababu, inatoa dira ya Washington kisiasa na pia kuonyesha namna utawala wa Trump ulivyojipanga kukabiliana na changamoto zinazokabili taifa hilo.
Rais Trump anatumia hotuba yake ya hali ya taifa kutetea misako yake ya uhamiaji, kupunguza gharama za matumizi katika serikali ya shirikisho, shinikizo lake la ushuru wa kimataifa ambao Mahakama ya Juu imeufuta, na uwezo wake wa kuongoza operesheni za kijeshi zinazofanywa ulimwenguni, ikiwa ni pamoja na Iran na Venezuela.
Rais na chama chake cha Republican wanaonekana kuwa hatarini, huku kura za maoni zikionyesha kuwa Wamarekani wengi hawaamini jinsi Trump alivyoiendesha serikali katika mwaka wake wa kwanza tangu aliporudi madarakani.
Lakini Mrepublican huyo anatumai kwamba anaweza kuwashawishi Wamarekani wanaozidi kuwa na wasiwasi kwamba sera zake zimeboresha maisha yao huku akihakikisha kwamba uchumi wa Marekani una nguvu zaidi kuliko wengi wanavyoamini — na kwamba wanapaswa kuwapigia kura katika uchaguzi wa katikati ya muhula mwezi Novemba.
Kurejesha "Ndoto ya Marekani”
Mada kuu ya hotuba yake ni kwamba nchi hiyo inazidi kukua kutokana na ongezeko la viwanda vya ndani na ajira mpya, licha ya Wamarekani wengi kutohisi hivyo.
Trump amesema na hapa namnukuu: "Baada ya mwaka mmoja tu, naweza kusema kwa heshima na fahari kwamba tumefikia mabadiliko ambayo hayajawahi kuonekana hapo awali,”
Tayari alikuwa ameahidi kuwa hotuba yake itakuwa ndefu kwa sababu ana mengi ya kuzungumzia na hasa kuhusu uchumi wa Marekani.
Rais amewaambia Wamarekani kuwa Warepublican ndio wanaofaa zaidi kuendelea kushughulikia wasiwasi wa umma kuhusu gharama ya maisha.
Trump amesema kwamba kama atapewa miaka mitatu zaidi katika Ikulu ya White House na akiwa na Warepublican huko Capitol Hill, wanaweza hatimaye kufikia tena kile kinachofahamika kama "Ndoto ya Marekani” ambayo walikuwa nayo katika muhula wake wa kwanza lakini ikapotea kwa sababu ya Joe Biden na Wademokrat katika kipindi cha miaka minne iliyopita.
Wademocrat washambuliwa
Huku wabunge wakikusanyika kusikiliza hotuba yake, Wizara ya Usalama wa Ndani bado imefungwa, baada ya ufadhili wake kuisha mnamo Januari 30.
Trump amewalaumu Wademokrat kwa kufungwa kwa shughuli za wizara hiyo, ambao wamekuwa wakisisitiza mabadiliko ya utendaji wa sheria wa maafisa wa uhamiaji wa shirikisho kabla ya kukubali kufadhili wizara hiyo.
Maafisa wa White House wamekuwa wakibadilishana mapendekezo ya sera na viongozi wakuu wa chama cha Democratic, lakini pande zote mbili zimeonyesha kuwa haziko karibu kufikia makubaliano ya kuumaliza mkwamo huo.
Wademokrat wanapanga majibu ya hotuba hiyo ikiwemo kususia kikao hicho. Gazeti la New York Times lilisema kiasi ya Wademokrat 40 walipangwa kususia hotuba hiyo.
Sera ya kigeni
Hotuba ya Trump inajiri wakati manowari mbili za Marekani za kubeba ndege zimepelekwa Mashariki ya Kati huku kukiwa na mvutano na Iran kuhusu mpango wa nyuklia. Ameliambia Bunge kwamba "atakabiliana na vitisho" vinavyolikumba taifa.
Rais amesimulia jinsi mashambulizi ya anga ya Marekani yalivyoharibu uwezo wa nyuklia wa Tehran mwaka uliopita, na kusifu operesheni maalum iliyomwondoa madarakani Rais wa Venezuela Nicolas Nicolás Maduro, pamoja na utawala wake kuratibu usitishaji mapigano katika vita vya Israel na Hamas huko Gaza.
Lakini pia aliutia doa ushirikiano wa kijeshi wa Marekani na Jumuiya ya NATO, kutokana na juhudi zake za kuiteka Greenland kutoka Denmark na kushindwa kwake kuchukua msimamo mkali zaidi dhidi ya Rais wa Urusi Vladimir Putin katika kukomesha vita vyake nchini Ukraine. Jumanne ilikuwa kumbukumbu ya miaka minne ya vita vya Urusi na Ukraine.
Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio alifanya mkutano kuhusu Iran saa chache kabla ya hotuba ya Trump na "Kundi la wajumbe Wanane" - lililojumuisha viongozi wa Seneti na Baraza la Wawakilishi na kamati za ujasusi za mabaraza yote mawili ya Bunge.