1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump asema siku za karibuni zitakuwa muhimu kuelekea kupona

Sekione Kitojo
4 Oktoba 2020

 Rais wa Marekani Donald Trump amesema siku zijazo zitakuwa "mtihani halisi" katika kupona kwake mambukizi ya virusi vya corona, katika  ujumbe wa vidio alioweka katika ukurasa wa Twitter siku ya Jumamosi,(02.10.2020).

Walter Reed Militärhospital | Donald Trump Videobotschaft Covid-19
Picha: The White House via Reuters

Vidio hiyo kutoka kwa rais Trump , ambaye  anatibiwa  katika hospitali ya  jeshi, inakuja  baada  ya  taarifa zinazokinzana kusababisha  mkanganyiko kuhusiana  na  hali  yake  kiafya.

Trump alikuwa  amevaa suti bila tai  na  alikuwa  amekaa wakati akirekodi  ujumbe wake  huo. Alisikika kidogo akiwa anashindwa kuzungumza  na akipumua  kwa  taabu.

Rais Donald Trump wa MarekaniPicha: The White House via Reuters

"Nafikiri nitarejea hivi karibuni," alisema, na  kuongeza  kwamba anapambana  kupona virusi hivyo kwa  ajili  yake binafsi  na  pia kwa  dunia  kwa  ujumla.

"Ni lazima nirejee kwasababu  bado  tunapaswa  kuifanya  Marekani kuwa  kubwa  tena," alisema , akitumia kauli mbiu  ya kampeni yake.

Amesema  "anaanza  kujisikia  vizuri " lakini  siku  za hivi  karibuni zitakuwa  mtihani halisi  wa kupona kwake, na  amewashukuru waungaji  mkono  wake  wa  ndani  ya  nje  ya  nchi  hiyo kwa kumtakia  kupona haraka na "mapenzi yao makubwa."

Daktari wake Sean Conley aliwaambia  waandishi  habari  mapema kuwa   hali  ya  Trump inaendelea  vizuri, na  kusema  timu  ya madaktari "ina  furaha  kubwa  kwa  maendeleo  anayopitia  rais."

Watu wakimtakia rais Trump kupona kwa harakaPicha: Andrew Kelly/Reuters

Hali yake ilikuwa inatia wasi wasi

Hata  hivyo , chanzo  kingine  kimewaambia  waandishi  habari kwamba  ishara muhimu  za  Trump zilikuwa  zinatia wasi wasi.

"Ishara muhimu za  rais  katika  muda  wa  masaa  24 zilikuwa zinatia  wasi  wasi  mno na  masaa 48 mengine yatakuwa  muhimu kwa maana  ya huduma  anayopewa. Bado  hatuko katika  njia  ya wazi  kuelekea  kupona  kabisa ," chanzo  hicho kimewaambia waandishi  habari  wa  Ikulu  ya  Marekani  ya  White House wanaosafiri  pamoja  na  rais.

Taarifa  hiyo iliyotolewa  na  chanzo  hicho  ilikuwa  inakanganya, wakati  inakuja  dakika  chache  baada  ya  madaktari  kutoa  taarifa kwa  umma, na  ilitolewa  kwa  masharti ya  kutotajwa jina. Ikulu  ya White House imekataa  kusema  lolote  zaidi.

Kituo cha  televisheni  cha  FOX wakati  huo huo  kimeripoti kuwa Trump alionesha "hali  ambayo  si  nzuri" za kupona kutoka  hali  ya kawaida  hadi mbaya kabla ya kupelekwa  katika  kituo  cha  afya cha  Walter Reed, kituo  cha  afya  cha  jeshi nje  ya  mji  wa Washington, siku  ya  Ijumaa.

Mtaalamu wa masuala ya mapafu sean Dooley akitoa maelezo juu ya hali ya rais Domald Trump katika kituo cha afya cha jeshi, Oktoba 3, 2020Picha: Brendan Smialowski/AFP/Getty Images

Hata  hivyo , ripoti  hiyo imemnukuu afisa  mwandamizi  wa  utawala huo  akisema kwamba "katika  muda wa  masaa 12 yaliyopita hakukuwa  na  wasi  wasi  kabisa."

Kumekuwa pia  na  ukosefu wa  uwazi  juu  ya  muda  wa maambukizi  ya  rais  huyo  pamoja na lini  alipimwa.