1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Trump ashikiliwa na kupigwa picha ya rekodi za polisi

Sylvia Mwehozi
25 Agosti 2023

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump ameshikiliwa kwa muda katika gereza la Fulcon huko Georgia baada ya kujisalimisha mwenyewe katika mashitaka yanayohusu njama za kutaka kubadili matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2020.

Donald Trump - Gereza la kaunti ya Fulton
Picha ya Trump aliyopigwa baada ya kushikiliwa na polisi Picha: Fulton County Sheriff's Office/Getty Images/AFP

Katika tukio hilo lililodumu chini ya dakika 30, Trump mwenye umri wa miaka 77, alishikiliwa na maafisa wa polisi kwa makosa 13 katika gereza la kaunti ya Fulton mjini Atlanta.

Mchakato huo unamaanisha kwamba taarifa kuhusu Trump kama mtuhumiwa wa uhalifu, zimeingizwa kwenye mfumo wa jela baada ya kushikiliwa na polisi.

Trump amepewa nambari ya mfungwa "PO1135809" na jela ya kaunti ya Fulton, ambayo imeorodhesha urefu wake kuwa futi sita inchi tatu, uzito wake kama kilo 97 na rangi ya nywele zake kama "Blond au Strawberry."

Bilionea huyo alichukuliwa alama za vidole na kupigwa picha ya rekodi za polisi za wahalifu na kisha kutoa dhamana ya Dola laki 200,000 na masharti mengine ili kuachiliwa.

Msafara wa Trump ukiwasili gereza la FulconPicha: Ricardo Arduengo/REUTERS

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukamatwa, Trump, alisema kuwa ilikuwa "siku ya huzuni sana kwa Marekani" na kuwashutumu wapinzani wake wa chama cha Democratic kwa "kuingilia uchaguzi."

Mashitaka hayo ni ya nne ya jinai dhidi ya Trump tangu mwezi Machi, alipokuwa rais wa kwanza wa zamani katika historia ya Marekani kufunguliwa mashtaka.

Trump na watuhumiwa wenzake 18 walishitakiwa mapema mwezi huu jimboni Georgia kwa tuhuma za kutaka kubatilisha matokeo ya uchaguzi. Kuelekea kura ya uchaguzi wa mwaka 2020, Trump alirekodiwa akiwashinikiza maafisa wa Georgia kumtafutia kura mpya katika jimbo hilo lenye ushindani.

Soma pia: Donald Trump kujisalimisha Alhamisi mahakamani Georgia

Baadhi ya washitakiwa wenzake wanatuhumiwa kufanya ulaghai kuwa wapiga kura rasmi na kutia saini vyeti bandia vya uchaguzi ili kumpendelea Trump.Ulinzi mkali ulikuwa umeimarishwa wakati Trump alipofika katika gereza la kaunti ya Fulton.

Baadae maafisa wa gereza wamechapisha picha ya Trump aliyopigwa katika rekodi za uhalifu naye pia akaichapisha katika ukurasa wake wa Truth Social na kuandika maneno haya "Uingiliaji Uchaguzi".

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW