Trump asikika akimtaka afisa wa uchaguzi 'kumtafutia kura'
4 Januari 2021Katika kanda hiyo ya sauti, Rais Trump anasikika akimuambia kamishna wa uchaguzi katika jimbo la Georgia Brad Raffensperger, kumtafutia kura 11,780, ambazo zingeweza kubadilisha matokeo na kumpokonya ushindi rais mteule Joe Biden katika jimbo hilo la Kusini mashariki.
Trump alisema, ''Watu wa Georgia wana hasira, watu wa nchi hii wana hasira, hutakuwa umefanya kosa lolote ukisema, unajua, uh, kwamba mmehesabu upya kura.''
Soma zaidi: Trump kuondoka ikulu baada ya Biden kuthibitishwa mshindi
Katika mazungumzo hayo mazima, Raffensperger na wakili wake wanasikika wakimfahamisha Trump kwamba madai yake kuwa amelishinda jimbo la Georgia yana msingi katika nadharia za uzushi ambazo zimethibitishwa kuwa za uongo, na kumhakikishia kuwa kura 11,779 ambazo Biden amemzidi Trump zilikuwa halali.
Njama za Trump zazidi kuanikwa kweupe
Kuchapishwa kwa mazungumzo hayo na gazeti la Washington Post ni ufichuzi wa juhudi nyingine ambazo Trump amekuwa akizifanya kwa miezi miwili iliyopita, kutaka kuwaaminisha watu kuwa kushindwa kwake na Joe Biden kulitokana na hila za wizi wa kura.
Madai hayo ya udanganyifu katika uchaguzi ambayo yanaendelezwa na Rais Donald Trump na washirika wake yametupiliwa mbali na maafisa wa uchaguzi wa majimbo na kesi zao nyingi zimetupwa nje na mahakama.
Soma zaidi:Wafuasi wa Trump waandamana wakidai udanganyifu wa uchaguzi
Katika ripoti yake ya jana Jumapili, gazeti la Washington Post limesema Trump alijaribu kila njia kuwashawishi na kuwatisha Raffensperger na maafisa wengine, akisema wanaweza kukumbwa na athari za kihalifu.
Shirika la habari la Associated Press limemnukuu Bob Bauer, mshauri mkuu wa rais mteule Joe Biden, akisema kanda hiyo ni uthibitisho usiopingika kwamba Trump aliwashinikiza maafisa wa chama chake kubatilisha matokeo halali ya uchaguzi na badala yake kuhalalisha yaliyopatikana kwa njia za wizi.
Sauti za ukosoaji dhidi ya Trump zaongezeka
Kabla ya gazeti la Washington Post kuyachapisha mazungumzo hayo, Trump aliandika katika mtandao wa twitter kwamba alizungumza kwa simu na kamishna wa uchaguzi wa jimbo la Georgia, na kudai kuwa kamishna huyo, ama hakutaka, au alishindwa kujibu maswali yanayohusiana na wizi wa kura.
Soma zaidi: Joe Biden athibitishwa rasmi kuwa rais ajae wa Marekani
Kamishna huyo mbaye kama Rais Trump anatoka katika chama cha Republican, alijibu kupitia mtandao huo huo, akisema, ''Kwa heshima zote bwana rais, unayoyasema ni uongo, ukweli utajulikana hivi punde''.
Huku hayo yakiiarifiwa, mawaziri wote 10 wa zamani wa ulinzi walio hai, wakiwemo kutoka chama cha Republican na kile cha Democratic, wamechapisha makala ya pamoja katika gazeti la Washington Post, wakimkanya na kumuonya Rais Trump asijaribu kuliingiza jeshi la taifa katika masuala ya kisiasa, wakisema hatua kama hiyo inaweza kuliingiza taifa lao katika mzozo ambao halijawahi kuushuhudia.
ape, https://p.dw.com/p/3nTga