1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump asimangwa kwa kauli yake

Admin.WagnerD13 Julai 2018

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May na rais wa Marekani Donald Trump watakuwa na mazungumzo kuhusu mahusiano ya kibiashara siku zijazo, licha ya Trump kumkosoa May kuhusu mpango wa Brexit, kauli iliyokasirisha wengi.

Großbritannien | May empfängt Trump zu Galadinner in Blenheim Palace
Picha: picture-alliance/ZumaPress/J. Goodman

Ukosoaji huo umewakasirisha Waingereza ambapo mmoja wa manaibu waziri kwenye serikali ya May amemtaka Trump kujifunza adabu. 

Kwenye mtandao wake wa Twiiter, Sam Gyimah, naibu waziri mdogo wa masuala ya utafiti katika vyuo vikuu na sayansi Uingereza, amemuuliza Rais Trump adabu zake ziko wapi. Kauli za Trump wakati akizungumza na gazeti la udaku The Sun linalounga mkono Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya, zimegonga vichwa vya habari nchini Uingereza, huku wanasiasa na wananchi wakimkosoa.

Trump akosoa May

Katika mkesha wa mkutano kati yake na Theresa May, Trump alisema kuwa hatua ya Uingereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya huenda itavunja matumaini ya mahusiano ya kibiashara kati ya mataifa hayo, akimlaumu waziwazi Bi May kwa kile alichokiita "kuburuzwa na Umoja wa Ulaya kinyume na matakwa ya wananchi wake walioamua kujiondoa kwenye Umoja huo."

Rais Donald Trump Picha: picture-alliance/P.M.Monsivais

Hata hivyo, waziri wa fedha wa Uingereza Phillip Hammond amesema; "Trump hajawa na nafasi ya kufanya mazungumzo na waziri huyo mkuu, lakini ana matarajio makubwa ya kupata fursa hiyo. Mazungumzo hayo yatalenga kutazama jinsi ya kupanua biashara na uwekezaji kati ya Uingereza na Marekani." Hamond aliwaambia wanahabari kabla ya mkutano na mawaziri wa fedha wa mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya jijini Brussels.

Trump aliliambia gazeti hilo la The Sun linalomilikiwa na bilionea mwenzake, Rupret Murdorch, "yeye angekuwa na mtazamo tofauti kuhusu suala hilo." Trump alimshauri May lakini ushauri wake hukuzingatiwa, kwa mujibu wa gazeti hilo. 

Baada ya juma gumu kwa May, wakati waziri wake kuhusu masuala ya Ulinzi David Davis na waziri wa masuala ya nje Boris Johnson kujiuzulu wakipinga mpango wa kujiondoa kwa uingereza kwenye Umoja wa Ulaya, Trump alimiminia sifa Johnson akisema kuwa angetekeleza kazi nzri kama waziri mkuu.

Waadamanaji wapinga ziara ya Trump

Matamshi kama hayo kwa rais wa Marekani ambaye yuko ziarani Uingereza kunamdhalilisha May, chama chake na taifa lake kwa jumla.

Baluni kubwa inayotumiwa kumkejeli rais Trump, Uingereza Picha: picture-alliance/ZUMA/London NEws Pictures/J. Goodman

Thamani ya sarafu ya Sterling ilidorora baada ya matamshi ya Trump. Alipoulizwa kuhusu matamshi hayo, msemaji wa May, alisema kuwa atafanya kikao na rais huyo wa Marekani na kujadili msimamo huo wake.

Wengi wametaja mpango wa May kuwa usaliti wakiwemo wabunge kwenye chama chake cha kihifadhina kilichogawanyika, ambao wameonya kuwa huenda akakabiliwa na changamoto za uongozi.

Msemaji wa ikulu ya White House Sarah Sanders amesema; "rais anamheshimu sana waziri huo mkuu;" akiongeza kuwa alisema kwenye mahojiano, "May ni mtu muungwana na kwamba hakusema kitu chochote kibaya kumuhusu yeye."

Huku hayo yakijiri waandamanaji wanapanga kumsimanga rais Trump wakitumia baluni kubwa katika barabara za London, wakimchora kuwa mtoto anayelia. Wanapinga ziara yake nchini Uingereza.

Mwandishi: Shisia Wasilwa, Ap, Reuters,

Mwandishi: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW