1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

Trump asitisha kushambulia vituo vya nishati vya Iran

23 Machi 2026

Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kusitisha kwa siku tano mashambulizi ya kijeshi dhidi ya miundombinu ya nishati ya Iran, baada ya kile alichokitaja kuwa mazungumzo yenye tija ya kumaliza vita vya Iran.

Washington D.C. Marekani 2026 | Donald Trump kabla ya kuondoka Ikulu ya Marekani kwa helikopta ya ‘Marine One‘
Trump hakutoa maelezo ya kina kuhusu mazungumzo hayo yaliyomfanya alegeze msimamo baada ya kitisho cha kushambulia vituo vya nishati vya IranPicha: Brendan Smialowski/AFP/Getty Images

Tangazo la Trump limejiri baada ya hapo awali kutishia "kuangamiza" miundo mbinu ya nishati ya Iran endapo Iran ingeendelea kuufunga mlango wa bahari Hormuz  

Trump aliandika tangazo hilo kwenye ukurasa wake wa mitandao ya kijamii Truth Social, saa kadhaa kabla ya muda wa mwisho aliotoa kama masharti kwa Iran kufungua mlango wa Bahari Hormuz kufika la sivyo ashambulie miundo mbinu zake za nishati.

Trump amesema Marekani na Iran zimekuwa na "mazungumzo mazuri na yenye tija" yanayoweza kuchochea makubaliano na suluhisho kamili la vita.

Kulingana na Trump, mjumbe wake maalum wa Mashariki ya Kati Steve Witkoff na mkwe wake Jared Kushner walifanya mazungumzo Jumapili hadi jioni, na mazungumzo hayo yataendelea wiki nzima.

Ameongeza kuwa kwa vyovyote vile ni sharti Iran iachane na urutubishani urani. Trump amesema mazungumzo hayo yanaendelea kufanywa na "afisa wa juu" wa Iran lakini si kiongozi mkuu wa nchi hiyo Ayatollah Mojtaba Khamenei. Akizungumza na waandishi Habari JUmatatu, Trump amesema: 

"Tumeuangamiza uongozi katika ngazi ya kwanza, ngazi ya pili, na kwa kiasi kikubwa ngazi ya tatu. Lakini tunazungumza na mtu ambaye naamini ndiye anayeheshimika zaidi na ni kiongozi."

Iran yakana kuzungumza na Marekani kuhusu usitishaji vita

Lakini wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imekana kufanya mazungumzo na Marekani.

Gazeli linalomilikiwa na serikali ya Iran- IRAN limeripoti kwamba kauli za Trump ni sehemu ya juhudi za kupunguza bei ya nishati, na kurefusha muda wa kutekeleza mipango yake ya kijeshi.

Vyombo viwili vya habari vya Iran vilivyo karibu na jeshi la Askari wa Mapinduzi nchini Iran vimedai kwamba hakujawa na mazungumzo ya moja kwa moja au ya njia za pembeni kati ya Tehran na Washington kama alivyoeleza Trump.

Badala yake, vyombo hivyo Fars na Tasnim vilimuonesha Rais Trump kama anayelegeza msimamo kutokana na vitisho vya Iran.

Mwanadiplomasia mkuu wa Oman Bad Albusaidi amesema nchi yake, ambayo kwa muda mrefu imewapatanisha Marekani na Iran, inafanya juhudi kuhakikisha usafiri salama kupitia Mlango Bahari wa Hormuz, lakini bila ya kutoa maelezo zaidi.

Bad Albusaidi ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman pia aliandika kwenye mitandao ya kijamii kwamba Iran haipaswi kulaumiwa kwa vita hivyo.

Kansela wa Ujerumani azungumza na Trump kuhusu kushambulia vituo vya nishati Iran

Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz amesema leo Jumatatu kwamba katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Rais Trump jana Jumapili, walizungumza kuhusu kitisho cha kushambulia miundombinu ya nishati ya Iran

Safari za ndege zavurugika Mashariki ya Kati

02:00

This browser does not support the video element.

"Nilimueleza wasiwasi wangu kuhusu mashambulizi yaliyotangazwa dhidi ya vituo vya umeme nchini Iran. Ninashukuru kwamba leo amesema atasitisha suala hilo kwa siku tano na sasa pia anafungua mlango wa uwezekano wa mazungumzo ya haraka na ya moja kwa moja na uongozi wa Iran.”

Japo nchi mbalimbali zimejaribu kupendekeza hatua za kutuliza mzozo huo ambao umetanuka kote Mashariki ya Kati, jibu la Iran limekuwa wazi: kwamba haikuanzisha vita. Kwa hivyo mapendekezo hayo yanapaswa kuelekezwa Washington” Hayo ni kulingana na gazeti la IRAN.

Iran yatishia kulipiza kisasi dhidi ya Marekani vituo vyake vya nishati vikishambuliwa

Awali, Iran ilitishia kushambulia miundo mbinu ya nishati katika nchi za Ghuba ambazo ni washirika wa Marekani kama kulipa kisasi endapo Marekani itatekeleza tishio lake au itatuma wanajeshi kuivamia.

Idadi ya vifo kutokana na vita hivyo imepita 1,500 ndani ya Iran, zaidi ya watu 1,000 nchini Lebanon, 15 nchini Israel na 13 wa Marekan wakiwemo wanajeshi. Isitoshe mamilioni ya watu nchini Iran na Lebanon  wamelazimika kuyakimbia makaazi yao.

Muda mfupi baada ya tangazo la Trump, jeshi la Israel lilisema linafanya wimbi jingine la mashambulizi dhidi ya baadhi ya maeneo katika mji mkuu wa Iran- Tehran.

(APE,RTRE)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW