1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump atafakari amri mpya ya kuwapiga marufuku wageni

Caro Robi
11 Februari 2017

Rais wa Marekani Donald Trump amesema anatafakari kutoa amri mpya ya kuwapiga marufuku raia wa baadhi za nchi kuizuru Marekani baada ya amri yake ya awali kuhusu hilo kupingwa na mahakama ya juu.

Trump signs an executive order at the White House in WashingtonTrump signs an executive order at the White House in WashingtonTrump signs an executive order at the White House in Washington
Picha: Reuters/K. Lamarque

Mnamo tarehe 27 mwezi uliopita, Trump aliagiza raia wa Libya, Iraq, Iran, Somalia, Sudan, Syria na Yemen kupigwa marufuku kuingia Marekani kwasababu za kiusalama.

Katika mazunguzo na wanahabari ambayo hayakutarajiwa akiwa katika ndege ya jeshi la angani la Marekani Ijumaa jioni, Trump ametangaza uwezekano wa kutoa amri mpya ifikapo Jumatatu au Jumanne wiki ijayo. Hata hivyo hajatoa maelezo ya kina kuhusu marufuku hiyo mpya.

Alikuwa akielekea katika makaazi yake yaliyoko jimbo la Florida akiwa na Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe. Wazo la Trump la kutoa amri nyingine ya rais kuhusiana na suala la kuwapiga marufuku raia wa nchi za Kiislamu linakuja baada ya mahakama kuu ya rufaa iliyoko San Franciso kutoa uamuzi wa kupinga amri ya raia ya kuwazuia raia kutoka nchi hizo saba.

Amri mpya huenda ikawapa wakosoaji wa Trump ushindi kwa kuhoji kuwa alilazimika kubadilisha msiamo wake kuhusu sera yake kuu kama rais. Licha ya tangazo hilo la Trump, utawala wake huenda bado ukapinga uamuzi wa mahakama ya rufaa wa kuzuia marufuku hiyo dhidi ya wageni.

USA Besuch Shinzo Abe bei Trump in WashingtonUSA Besuch Shinzo Abe bei Trump in Washington
Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe na Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Reuters/J. Bourg

Marufuku hiyo ya awali ambayo Trump alidai lengo ni kuepusha mashambulizi ya kigaidi, ilisababisha mtafaruku mkubwa na kupelekea shutuma kali kutoka nchi zilizolengwa, nchi za magharibi na mashirika makubwa ya kibiashara ya Marekani hasa ya sekta ya teknolojia.

Jaji wa mahakama ya Seattle alisitisha agizo la kuwapiga marufuku wasafiri na wahamiaji kutoka nchi hizo saba na siku ya Ijumma wiki iliyopita, agizo hilo la mahakama lilithibitishwa na mahakama ya rufaa ya San Francisco na kusababisha kiongozi mpya wa Marekani kuandika maneno makali katika ukurasa wake wa Twitter akishutumu majaji na idara ya mahakama.

Maamuzi hayo ya mahakama yanaibua maswali kuhusu hatua ijayo ya Trump. Afisa wa ikulu ya rais aliye na ufahamu kuhusu mipango ya Trump amesema iwapo amri mpya itatolewa itahusisha mchango wa msaidizi wa Ikulu ya rais, Stephen Miller, ambaye alihusika katika amri ya awali pamoja na maafisa kutoka baraza la kitaifa la usalama, wizara ya sheria na ile ya usalama wa ndani.

Haijabainika ni kwa kiasi gani amri mpya ya rais itakavyoathiri kesi zilizowasilishwa mahakamani na walioathirika na amri ya awali. Hata hivyo kuna uwezekano amri mpya ya rais ikakumbwa na changamoto za kisheria na wanaoipinga wakaiomba mahakama kuwaruhusu kuyafanyia mageuzi malalamishi yao mahakamani.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/Ap

Mhariri: Yusra Buwahyid

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW