1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump ataka shule za umma kufunguliwa

28 Aprili 2020

Rais Donald Trump wa Marekani amesema serikali za majimbo nchini humo zinapaswa kufikiria kufungua shule za umma licha ya hofu ya usalama wa kiafya inayowakodolea macho wanafunzi kutokana na janga la virusi vya corona.

USA | Donald Trump | Coronavirus Briefing
Picha: Reuters/J. Ernst

 

Rais Trump alitoa kauli hiyo katika mkutano wa njia ya simu kwa magavana waliokuwa wakijadili jinsi ya kuruhusu tena shughuli za kiuchumi kuendelea miongoni mwa masuala mengine.

Amesema "Tunapendekeza wafungue shule haraka iwezekanavyo lakini kwa tahadhari na kuzingatia usalama. Tunataka kila mtu awe salama, nadhani mutaliona hilo. Magavana wengi wanafikiria kuhusu mifumo ya shule zao, si mbali shule zitafunguliwa tena hata kama ni kwa muda mchache. Nafikiria huenda likawa jambo zuri."

Hata hivyo kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press, hakuna gavana yoyote aliyeridhia pendekezo hilo la kufungua shule. Maafisa wengi wa elimu wana wasiwasi kuwa huenda kukawa na hasara kubwa hata kuliko faida iwapo shule zitafunguliwa.

Shule kote nchini Marekani zimefungwa kutokana na janga la virusi vya Corona.

India yafuta mpango wa kununua bidhaa za China

Wahudumu wa afya katika hospitali ya kitaifa ya Howrah, India wakiwa na barakoaPicha: DW/S. Bandopadhyay

Kwengineko, ubalozi wa China nchini India umekosoa vikali hatua ya India ya kuvitaja vifaa vya upimaji vilivyonunuliwa kutoka China kama visivyofaa.

Jana Jumatatu, India ilifuta ununuzi wa vifaa vya upimaji kutoka kampuni mbili za China baada ya kulalamika kuhusu ubora wake na bei, lakini msemaji wa ubalozi wa China nchini India, Ji Rong, alionekana kutetea ubora wa bidhaa za China kwa kusema nchi hiyo inazingatia ubora wa bidhaa wanazozitengeza na kuuza.

Rong amesisitiza kuwa kampuni hizo za China zilikidhi viwango vya ubora vilivyowekwa nchini humo na pia bidhaa hizo zilithibitishwa kuwa bora na mamlaka za India.

Mahakama ya New Delhi ilifutilia mbali mpango wa kununua vifaa hivyo vya upimaji wakitoa sababu kuwa walitakiwa kulipa zaidi ya mara mbili tofauti na bei ya kawaida.

Na nchini Italia, kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis ametoa wito kwa watu kuendelea kufuata utaratibu uliotolewa na serikali zao ili kupunguza kasi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Papa Francis alitoa wito huo baada ya maaskofu kadhaa wa Italia kulalamika kuhusu utaratibu uliotangazwa na serikali ya nchi hiyo wa kufungua shughuli za kiuchumi bila ya kutaja jinsi ibada za kanisa zitakapoanza tena.

Kupitia taarifa, maaskofu nchini humo wamesema hawatakubali uhuru wao wa kufanya ibada ukandamizwe.

Hali hiyo inadhihirisha uwepo kwa vuta nikuvute kati ya kanisa na serikali wakati huu ambapo serikali imeweka vizuizi ili kudhibiti kusambaa kwa virusi vya Corona.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW