Trump ataka Waislamu wapigwe marufuku Marekani
8 Desemba 2015Akizungumzia juu ya mashambulio ya kigaidi yaliyofanywa na watu waliokuwa na itikadi kali katika mji wa San Bernadino ,katika jimbo la California, Donald Trump ametoa mwito wa kuwapiga marufuku Waislamu wote nchini Marekani , wahamiaji na wale wanaotaka kuingia nchini Marekani. Trump amedai kwamba pana idadi kubwa ya Waislamu wanaowachukia Wamarekani.
Kauli ya Trump imemshutua Mkurugenzi wa baraza la uhusiano wa Marekani na waislamu Nihad Awad. Bwana Awad amesema kumsikia Donald Trump akitoa mwito wa kuwapiga marufuku Waislamu wote kuingia nchini Marekani ni jambo la kughadhbisha.
Amesema kauli hiyo ni ya kukasirisha, hasa ikiwa imetolea na mtu anaewania kuushika wadhifa wa juu kabisa nchini Marekani. Mkurugenzi huyo amesema Trump na wengine wanawapa rutuba magaidi wa dola la kiislamu.
Bwana Awad ameeleza kuwa alichokisema Donald Trump ndicho hasa ambacho magaidi wa dola la kiislamu wanachotaka kukisikia. Hata hivyo ametoa uhakika kwamba Waislamu hawatakubali kugawanywa.
Waislamu kutoka nje pia wamjibu Trump
Kauli ya Trump imejibiwa pia nje ya Marekani. Afisa kutoka ofisi ya Sheikhul nchini Thailand Somchai Jewangma ameeleza kuwa Marekani ina uhusiano wa kiuchumi na nchi za kiislamu na kwamba wapo Mamilioni ya Waislamu nchini Marekani.Ameeleza kwamba kuwapiga marufuku Waislamu kuingia Marekani ni jambo lisilowezekana.
Mwenyekiti wa kituo cha masuala ya kiislamu mjini Canberra Azra Khan ameeleza kwamba, njia anayoitumia mjumbe wa chama cha Republican, Trump, kutoa jibu la mauaji yaliyofanywa California siyo sahihi. Azra Khan amesema lengo la Trump ni kuuwasha moto. Bwana Azra amemshauri Trump apiganie bunduki zipigwe marufuku nchini Marekani.
Naibu waziri wa mambo ya ndani wa Malasia Nur Jazlan Mohamad ameilezea kauli ya Donald Trump kuwa kinyume cha maadili ya Marekani ya stahamala na demokrasia. Naibu Waziri huyo ametahadhrisha kuwa maneno aliyoyasema mgombea urais wa chama cha Republican yanaweza kutumiwa na magaidi wa dola la kiislamu ili kuwagawanya Waislamu.
Mgombea mwingine wa urais wa chama cha Republican Jeb Bush amemwita Donald Trump kuwa kichaa. Anaewania urais kwa tiketi chama cha demokratik Hillary Clinton ameeleza kuwa kauli ya Trump ni ya makosa.
Mwandishi:Mtullya Abdu/Ape/ rtre,
Mhariri: Iddi Ssessanga