1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump atangaza mageuzi ya sera ya uhamiaji Marekani

Sylvia Mwehozi
17 Mei 2019

Rais Donald Trump  wa Marekani  amewasilisha mapendekezo ya kuufanyia mageuzi mfumo wa sera ya uhamiaji ambao amesema utakuwa mfumo bora duniani kote huku ukihimiza fursa sawa miongoni mwa waombaji. 

U.S. President Trump delivers speaks about immigration reform at the White House in Washington
Picha: REUTERS

Trump amesema mfumo wa sasa "haufanyi kazi" na umegubikwa na matatizo, ikiwemo kuwapendelea watu walio na ndugu nchini Marekani chini ya sera ambayo imekuwepo kwa miongo kadhaa ikiruhusu watu wasio na thamani kupewa nafasi.

Katika hotuba yake aliyoitoa Ikulu ya White House, Trump anasema mfumo huo wa sasa hauwezeshi vibali kutolewa kwa madkatari, watafiti au wanafunzi walio na uwezo wa juu ambao wanahitimu katika vyuo nchini humo, baadhi yao wakirejea katika nchi zao kuanzisha biashara ambayo ingeanzishwa nchini humo. Soma zaidi...

"Lakini badala ya kuchagua watu kwa bahati nasibu tutaweka vigezo rahisi na vya kimataifa kwa ajili ya kuingia Marekani. Tutaondoa vigezo vya Green Card na kuweka visa mpya, visa ya kuijenga Marekani kwanza, ambayo ndio wote tunataka kusikia, alisema Trump.

Marekani tayari inawapatia vibali watu milioni 1.1 kwa mwaka au kibali cha kuishi Marekani maarufu kama "green card", ambavyo vinawaruhusu wapokeaji kuishi na kufanya kazi nchini humo. Asilimia 66 ya vibali hivyo hutolewa kwa watu walio na ndugu wanaoishi kihalali nchini humo na asilimia 21 hutolewa kibahati nasibu. Trump anasema mfumo mpya wa uhamiaji utaifanya Marekani kuwa shindani huku ukihakikisha nchi inaendelea kuwakaribisha wageni.

Uzio wa chuma mpakani mwa Marekani na MexicoPicha: picture-alliance/ZUMA Wire/C. Brown

Aidha amesema mipango yake ni kutengeneza nafasi za ajira, kipato na usalama wa wafanyakazi wa Marekani kwanza. Amezitolea mfano mifumo ya uhamiaji ya Canada, New Zealanda na Australia kama mifumo iliyo bora.

Suala la usalama katika mpaka na Mexico limekuwa kipaumbele katika utawala na anapendekezo matumizi ya teknolojia ili kuongeza usalama wakati utawala wake ukiendelea na ujenzi wa ukuta ambao umekuwa kiini cha mvutano kati yake na bunge.  Chini ya mapendekezo, waombaji sasa watalazimika kujifunza kiingereza na kufanya mtihani, akiongeza kwamba kwa namna hiyo mfumo utawanufaisha watu "walio na maarifa, wasomi na wahamiaji vijana".

Trump ana matumaini Wademocrats katika bunge wataungana naye kuunga mkono mageuzi hayo, ingawa majaliwa ya mapendekezo hayo kupitishwa na bunge na kuwa muswada bado hayakuwa wazi. Wakosoaji wanasema mpango huo mpya hautoi mwanga wa namna ya kuwashughulikia wahamiaji haramu ambao tayari wapo nchini humo au hatma ya watu walioingia Marekani wakiwa watoto na ambao wamekua bila ya uraia".

Spika wa bunge Nancy Pelosi amesema Marekani lazima iwe na mageuzi pana ya uhamiaji lakini akisema unaonekana mpango huo ni wa "kujionyesha bora".

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW