Marekani: Trump atangaza ushindi dhidi ya Harris
6 Novemba 2024Matokeo ya uchaguzi yamemuweka mgombea huyo wa Republican kifua mbele dhidi ya Mdemokrat Kamala Harris.
Akiwahutubia wafuasi wake mapema leo hata kabla ya vyombo vya habari kumtangaza mshindi, rais huyo wa zamani wa Marekani amesema huo ni ushindi wa kisiasa ambao Marekani haijawahi kuushuhudia.
"Ahsanteni sana. Hii inapendeza. Tuna maelfu ya marafiki kwenye vuguvugu letu hili. Hili likuwa vuguvugu ambalo halijawahi kushuhudiwa. Na, kwa kweli, hili lilikuwa, naamini, vuguvugu kubwa kabisa la kisiasa la wakati wote. Na sasa litakuwa muhimu hata zaidi kwa sababu litatusaidia kuliponya taifa letu."
Soma pia:Donald Trump: Wamarekani mmefanikisha ushindi
Televisheni za Marekani zimesema Trump mwenye umri wa miaka 78 ameshinda majimbo ya maamuzi ya Pennsylvania, Georgia na North Carolina.
Katika pigo jingine kwa Wademocrat, chama cha Trump cha Republican pia kimekamata udhibiti wa baraza la Seneti.
Viongozi wa ulimwengu tayari wanatuma salamu zao za pongezi kwa Trump, wakiwemo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na viongozi wa madola makubwa ya Ulaya pamoja na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Mark Rutte.