1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump atengwa katika maamuzi ya mkutano wa G20

Daniel Gakuba
8 Julai 2017

Nchi 19 kati ya 20 katika mkutano wa G20 zimezungumza kwa kauli moja kuhusu biashara na kulinda mazingira. Sera za Rais wa Marekani Donald Trump zimemuacha peke yake, bila mshirika hata mmoja.

G20 Gipfel in Hamburg | Angela Merkel, Bundeskanzlerin
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akiuhitimisha mkutano wa G20 HamburgPicha: Reuters/A. Schmidt

Tangazo kuhusu maazimio yaliyofikiwa katika mkutano huu wa kundi la nchi zinazoongoza kiviwanda na zinazoinukia kiuchumi, linasema viongozi wameafikiana kuunga mkono kwa dhati mkataba wa Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi, na kuutekeleza kikamilifu. Akisoma tangazo hilo, mwenyeji na mwenyekiti wa mkutano huo, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, amesema viongozi wamelezea mshikamano katika kuutekeleza kikamilifu mkataba wa Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi, unaopingwa na utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani.

Amesema, ''Kuhusu mkataba wa Paris juu ya Mabadiliko ya tabianchi, tumeeleza bayana malengo yetu ya kuutekeleza. Marekani imezungumzia msimamo wake, lakini nafurahi kuona viongozi wengine wote wakikubaliana kuwa mkataba huo wa Paris hautabadilika''.

Mwezi uliopita Rais Donald Trump aliiondoa Marekani katika mkataba wa Paris, akidai unahujumu uchumi wa nchi yake na sekta yake ya nishati.

Sera za Trump zaelezwa kuwa kinyume cha maslahi ya dunia

Ilikuwa kumi na tisa dhidi ya mmoja, mmoja akiwa TrumpPicha: Getty Images/U. Michael

Suala la kutunza mazingira ya dunia pamoja na kuondoa vizuizi vya biashara yamekuwa masuala yenye kuleta mgawanyiko katika mkutano huu wa kilele, na masuala hayo mawili yamechukua muda mwingi wa maafisa ambao wamekuwa wakifanya kazi usiku kucha kutafuta muafaka.

Bi Angela Merkel amesema katika tangazo hilo kuwa kwa kauli moja viongozi wa nchi 19 kati ya 20 zinazounga kundi la G20 wamekubaliana kuwa vuguvugu la mataifa kujitenga na mchakato wa utandawazi, ambalo rais Trump analaumiwa kulifuata katika sera yake ya Marekani kwanza, linakwenda kinyume na maslahi ya uchumi wa dunia na kuhakikisha utengamano wa kifedha kwa ngazi ya dunia.

Lakini katika kuujumuisha msimamo wa Marekani katika tangazo la kuhitimisha mkutano huo, viongozi wa G20 wamesema katika kuondoa vipingamizi vya biashara huria, watakakisha maslahi ya kila upande yanalindwa, na kutambua hatua halali za nchi kulinda masoko yao.

Maandamano ya ghasia yameuandama mkutano huu tangu mwanzo hadi mwishoPicha: Reuters/H.Hanschke

Rais Trump amekuwa akilaani vikali mfumo wa sasa wa biashara, akidai anaigharimu Marekani nafasi za ajira kwa watu wake.

Hatutaiacha nyuma Afrika-Merkel

Kansela Angela Merkel amezungumzia pia azma ya nchi za G20 kuisaidia Afrika kusonga mbele kiuchumi.

Pia tumezingatia mpango wa Ujerumani wa kutoa msaada mkubwa zaidi kwa Afrika, pamoja na kuzisaidia nchi za bara hilo chini ya msingi wa ushirikiano, kupitia kile kinachoitwa 'Compact for Africa', kwa kushirikiana sio tu na viongozi, bali pia kupitia uwekezaji wa binafsi.

Masuala mengine yaliyojadiliwa katika mkutano huu ni kuwapiga vita wasafirishaji haramu wa binadamu katika hatua za kupambana na mzozo wa wakimbizi, na pia kushirikiana kumaliza tatizo sugu la ugaidi

Tangu mwanzoni mkutano huu wa kilele wa G20 mjini Hamburg uliandamwa na maandamano ya makundi yanayopinga utandawazi, ambayo mara kadhaa yaliishia katika ghasia zilizowajuruhi watu wengi, wakiwemo maafisa wa polisi zaidi ya 200.

Kansela Merkel amezilaani ghasia hizo, akisema ingawa anatambua uhuru wa watu kuandamana, vitendo vya fujo havikubaliki kwa sababu vinayaweka hatarini maisha ya watu na mali zao.

Mwandishi: Daniel Gakuba/dpae, rtre

Mhariri: Mohammed Abdul-rahman

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW