Trump atetea haki yake ya uhuru wa kujieleza
8 Agosti 2023Akitumia mtandao wake wa kijamii Truth Social kuelezea hali ya sasa, Trump ameandika: "Sipaswi kuwekewa amri ya kuzuiliwa cha kusema kwa sababu huko kutakiuka haki yangu ya uhuru wa kusema. Badala yake, wa kuwekewa vizuizi hivyo ni Wizara ya Sheria ambayo imekuwa ikivujisha kila kitu."
Katika hati iliyowasilishwa mahakamani hapo jana, mawakili wa kiongozi huyo wa zamani wa Marekani wamesema vikwazo vinavyopendekezwa na upande wa mashitaka vinakinzana na katiba ya Marekani.
Mmoja wa mawakili hao, John Lauro, amesema ni ajabu kwamba kwenye kesi ambayo inahusiana na haki za kikatiba, upande wa serikali unataka mahakama kuminya haki za kikatiba.
Waendesha mashitaka walimuomba Jaji Tanya Chutkan, ambaye ndiye atakayeendesha kesi hiyo, kuwapatia amri ya kumuwekea Trump mipaka ya kipi anaweza na kipi hawezi kukiweka hadharani, baada ya rais huyo wa zamani kuandika ujumbe wa vitisho siku ya Ijumaa kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social kwamba: "Ukiniandama, nakuandama!"
Soma pia: Trump kuomba kubadilishiwa jaji
Kwa mujibu wa waendesha mashitaka, vizuizi wanavyoviomba ni muhimu kwenye kesi hii kwa kuwa Trump amekuwa akitoa kauli zinazowajengea taswira mashahidi, majaji, wanasheria na wote wanaohusika na mambo ya kisheria kuwa wapo dhidi yake.
Upande wa mashitaka unahofia kwamba Trump anaweza kutumia mitandao ya kijamii kuchapisha nakala za mwenendo wa kesi na nyaraka nyengine za siri ambazo zinaweza kuathiri matokeo ya kesi yenyewe.
Mawakili wa Trump wapinga amri hiyo
Hata hivyo, wakili wa Trump, John Lauro, amesema kwamba kauli ya mteja wake haikumaanisha kitisho kwa mtu yeyote mahsusi, isipokuwa ni kauli ya jumla ambayo haipaswi kutumiwa na upande wa mashitaka kutaka kumuwekea rais huyo wa zamani vikwazo vya kutumia haki yake ya kikatiba ya kujieleza.
Ombi hilo la upande wa mashitaka liliwasilishwa muda mchache baada ya Trump kurejelea ombi lake la kuondolewa kwa Jaji Chutkan kwenye kesi yake. Trump alisema siku ya Jumapili kuwa hawezi kupata haki yake chini ya jaji huyo aliyeteuliwa na mtangulizi wake, Rais Barack Obama kutokea chama cha Democrat.
Soma pia: Trump akana mashitaka yanayohusiana na uchaguzi
Badala yake alisema kwamba angeliomba kesi hiyo ihamishwe kutoka mji mkuu, Washington, ambako anadai kuwa majaji wa mji huo wanaegemea upande wa wapinzani wake wa Democrat. Jaji Chutkan mwenye umri wa miaka 61 ana historia ya kuwa pande tafauti kisheria na Trump, baada ya kutoa hukumu dhidi yake mwezi Novemba 2021, ambapo aliandika kwenye hukumu yake kuwa "marais si wafalme."
Trump amekuwa akikana mashitaka ya jinai yanayomkabili, juu ya kuhusika kwake katika njama za kutaka kutengua matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2020 na kuwalaghai Wamarekani.
(AFP,AP)