1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump atishia kuiondoa Marekani WTO

Isaac Gamba
31 Agosti 2018

Rais wa Marekani, Donald Trump amesema kuwa anafikiria kutangaza kuiondoa Marekani katika Shirika la Biashara Duniani, WTO iwapo hakutafanyika mageuzi yanayolihusu shirika hilo.

USA Donald Trump
Picha: picture-alliance/newscom/UPI Photo/K. Dietsch

Akizungumza jana, Trump amesema WTO imekuwa haiitendei haki Marekani na kulilamu shirika hilo kuruhusu hali hiyo kutokea. Amesema hali hii inaendana na hatua ya mataifa kadhaa kutishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Marekani kupitia WTO  kuhusiana na vita vya kibiashara vya Marekani. 

Hayo yanajiri wakati ambapo Marekani na Urusi zikilaumiana kuhusu hatua ya nchi zote mbili kila moja kupandisha ushuru kwa bidhaa za chuma cha pua pamoja na bati.

Iwapo Marekani itajiondoa WTO basi hatua hiyo inaweza kusabaisha sintofahamu kufuatia hatua ya Trump kutangaza kodi kwenye bidhaa za chuma cha pua na bati zinazotoka nchi washirika za Umoja wa Ulaya, Mexico, Canada na China. 

Awali Waziri wa Biashara wa Marekani, Wilbur Ross alikieleza kituo cha matangazo cha CNBC kuwa ni mapema mno kujadili kujiondoa WTO, licha ya kusisitiza kuwa chombo hicho kinahitaji mageuzi makubwa.

Trump amekuwa akiikosoa WTO na mara nyingi akilalamikia sera za kibiashara za washirika huku akisisitiza kujadili upya makubaliano ya kibiashara yaliyopo kati ya Marekani na washirika.

Uholanzi moja ya nchi zenye mgogoro wa kibiashara na Marekani

 

Shirika la kimataifa la biashara WTOPicha: picture-alliance/dpa/Xinhua/X. Jinquan

Uholanzi ni moja ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya ambayo imekuwa na mgogoro wa kibiashara na Trump unaohusu mauzo ya vifaa vya magari.

Trump ameiagiza wizara yabiashra ya Marekani kufuatilia iwapo kuna haja ya kuongeza kodi zaidi katika magari, malori na vifaa vya magari yanayoingizwa nchini humo kutoka Umoja wa Ulaya na katika mataifa mengine, hatua iliyosababisha Umoja wa Ulaya kuonya kuwa utalipiza kisasi na hatua hiyo itaigharimu Marekani kiasi cha dola karibu dola bilioni 300.

Wakati wa mkutano kati yake na Waziri Mkuu wa Uholanzi, Mark Rutte, Trump alisema alikuwa anakaribia kufikia makubaliano ya mikataba kadhaa ya kibiashara akisema ni mikataba yenye maslahi kwa pande zote na kuongeza kuwa Marekani itaendelea kufanya mazungumzo na Umoja wa Ulaya kuhusiana na masuala ya kibiashara.

Alisema mazungumzo hayo yatajikita katika masuala ya kazi na usalama.

Kumekuwepo na dalili za mvutano katika ikulu ya Marekani kuhusu jinsi ya kuyashughulikia masuala ya kibiashara ikiwa ni pamoja na mvutano kati ya Marekani na China kuhusu biashara.

Wiki iliyopita Ikulu ya Marekani iliunga mkono hoja ya kuwawekea vikwazo vikali raia wa China wanaowekeza Marekani.

Mwandishi: Isaac Gamba/APE/DPAE

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW