Trump aitishia tena Iran licha ya makubaliano
17 Juni 2026
Mengi yanaanza kuibuka kuhusu kilichomo kwenye makubaliano ya kuelekea usitishaji vita vilivyoanzishwa na Marekani na Israel dhidi ya Iran yanayotazamiwa kusainiwa siku ya Ijumaa (Juni 19) nchini Uswisi, likiwemo la Iran kurejeshewa dola bilioni 300 zinazoshikiliwa kwenye orodha ya vikwazo vya Marekani dhidi yake.
Lakini kauli na misimamo inayobadilikabadilika ya Rais Donald Trump wa Marekani na operesheni ya kijeshi ya Israel nchini Lebanon vinahofiwa kuwa kigingi cha kusainiwa makubaliano hayo.
Siku ya Jumatano (Juni 17) Rais Trump alizuka tena na vitisho dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, akitishia kuipiga tena mabomu.
Akiwa na Rais Abdulfattah al-Sisi wa Misri kandoni mwa mkutano wa kilele wa mataifa saba yenye nguvu zaidi duniani mjinji Evian, Ufaransa, Trump alisema: "Ikiwa Wairani hatawakuwa na adabu vizuri, tutarudi kwenye kuwavurumishia mabomu vichwani mwao."
Ambapo kauli kama hizi si mpya kutolewa na kiongozi huyo wa Marekani, wachambuzi wanahofia kuwa huenda zikapunguza morali ya Wairani kuelekea kusainiwa makubaliano hayo.
Sehemu kubwa ya tabaka linalotawala mjini Tehran halikubaliani na suluhu yoyote isipokuwa vita, ambavyo wanadai vililazimishwa kwao pale Februari 28 wakati Washington na Tel Aviv zilipoanzisha operesheni ya mauaji na mashambulizi kote nchini Iran.
Iran kupata dola bilioni 300
Makubaliano hayo, ambayo tayari yameshasainiwa kidijitali, yamepangiwa kusainiwa kwenye makaratasi katika sherehe iliyoandaliwa nchini Uswisi sikuj ya Ijumaa, ambapo kwa upande wa Marekani, Makamu wa Rais JD Vance ndiye atakayeiwakilisha nchi yake. Ujumbe wa Iran kwenye hafla hiyo utaongozwa na Spika wa Bunge, Mohammad Bagher Qalibaf.
Sehemu ya makubaliano iliyovujishwa kwa baadhi ya mashirika ya habari inataja kuwa Iran itapata hadi dola bilioni 300 kutoka fedha zake zinazozuiliwa na Marekani.
Hata hivyo, makubaliano hayo yanaweza pia kuchafuliwa na operesheni ya kijeshi ya Israel inayoendelea nchini Lebanon.
Alfajiri ya Jumatano, jeshi la Israel lilishambulia maeneo kadhaa ndani ya ardhi ya Lebanon, licha ya maafisa wa Marekani na Iran kusisitiza kuwa makubaliano ya kusitisha yanaijumuisha Lebabon pia.
Israel yenyewe haijasema wazi endapo itakuwa sehemu ya makubaliano hayo, lakini siku ya Jumatatu, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alisema wanajeshi wake wataendelea kubakia ndani ya ardhi ya Lebanon kadiri wanavyohitajika.
Mafuta ya Iran yasafirishwa
Kwenyewe Iran, imeripotiwa kuwa meli zake za mafuta zimeondoka kwenye eneo la Ghuba ambalo lilikuwa limewekewa mzingiro na jeshi la Marekani.
Mtandao unaofuatia safari za meli za mafuta dunianil TankerTrackers, ulisema hii ni mara ya kwanza kwa Iran kusafirisha mafuta yake ndani ya kipindi cha miezi miwili.
Ripoti hiyo imekuja muda mchache baada ya naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Iran kusema kuwa mzingiro huo wa Marekani ulikuwa umeondoshwa.
Kwenye soko la dunia, bei ya mafuta imeshuka kidogo hadi dola 79 kwa pipa, huku ndani ya Marekani kwenyewe likifikia dola 76, mara ya kwanza kufika bei hiyo ndani ya kipindi cha miezi kadhaa.