1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump atishia kutumia jeshi kudhibiti waandamanaji

2 Juni 2020

Rais wa Marekani Donald Trump ametishia kupeleka maelfu ya polisi mjini Washington kudhibiti maandamano yanayoendelea, kufuatia mauaji ya mmarekani mweusi George Flyod yaliotokea akiwa mikononi mwa polisi.

USA Präsident Trump vor der St John's Church in Washington
Picha: Reuters/T. Brenner

Maandamano yameongezeka wiki moja baada ya kifo cha mmarekani mweusi George Floyd, mjini Minneapolis, aliyeuwawa na polisi mweupe Derek Chauvin wakati alipomuekea goti lake shingoni kwa takriban dakika 9, huku Floyd akisikika akisema hawezi kupumua.

Mauaji yake yamesababisha maandamano makubwa yaliojaa ghasia mjini New York, na miji mingine mingi nchini Marekani, maandamano ambayo hayajawahi kushuhudiwa kwa miongo kadhaa.

Baada ya kutuhumiwa kwa ukimya wake kufuatia hali inavyozidi kuwa mbaya nchini humo, Rais Donald Trump alizungumza kwa ukali katika hotuba yake kwa taifa siku ya Jumatatu kutoka Ikulu ya Marekani huku polisi wakisikika wakirusha mabomu ya kutoa machozi kwa waandamanaji nje ya Ikulu. Trump amesema atapeleka maelfu kwa maelfu ya wanajeshi watakaojihami kwa silaha nzito ili kudhibiti maandamano na kusitisha uporaji.

"Ndio maana nachukua hatua ya amri ya rais kusitisha machafuko na kurejesha usalama Marekani. Nakusanya raslimali zote za serikali, kiraia na kijeshi, kusitisha vurugu na uporaji, na kukomesha uharibifu na mashambulzii ya kuchoma moto," alisema Rais Trump.

Trump ameongeza kuwa iwapo magavana wa miji au majimbo hawatachukua hatua ya kulinda maisha na mali za watu wa eneo wanalolisimamia, atapeleka wanajeshi kusaidia kusawazisha hali. Licha ya tangazo lake, waandamanaji waliendelea na maandamano yao ya amani kupinga kile walichokiita ukatili wa polisi na ubaguzi wa rangi.

Joe Biden apinga tishio la Trump

Joe Biden makamu wa rais wa zamani nchini Marekani Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Rourke

Kwa upande wake Joe Biden mgombea wa kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa Novemba mwaka huu, amekosoa uamuzi wa Trump na kuandika katika mtandao wake wa twitter kwamba, Trump anatumia jeshi la Marekani, risasi za mipira na mabomu ya kutoa machozi dhidi ya watu wake, na kwamba ni lazima adhibitiwe.

Maandamano hata hivyo katika maeneo mengine ya Marekani yamekuwa ya amani na yamehudhuriwa pia na maafisa kadhaa wa polisi walioonekana kuwakumbatia na kuwapa moyo waandamanaji waliokuwa wanabubujikwa na machozi.

Huku hayo yakiarifiwa uchunguzi mpya uliofanywa kwa mwili wa George Floyd kufuatia ombi kutoka kwa familia yake,  umebaini Mmarekani huyo mweusi alikufa kutokana na damu kutotiririka vizuri mwilini kutokana na goti la polisi lililokuwa limekaba koo yake. Uchunguzi huo umezidisha miito ya waandamanaji ya kutaka maafisa wengine watatu waliohusika na kifo chake kushitakiwa.

George Floyd anatarajiwa kuzikwa wiki ijayo tarehe 9 Juni  mjini Houston mahali alikokulia nchini Marekani.

Kwengineko waandamanaji kutoka Australia na maeneo mengine ya Ulaya wameandamana kuonesha mshikamano na watu wa Marekani wanaodai haki kwa kifo cha Floyd, huku wakitaka serikali zao pia kushughulikia masuala ya ubaguzi wa rangi na ukatili wa polisi.

Vyanzo: afp/ap

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW