1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump ausitisha mpango wa DACA unaowalinda wahamiaji

Caro Robi
6 Septemba 2017

Rais wa Marekani Donald Trump ameufutilia mbali mpango uliowahakikishia takriban vijana 800,000 ambao waliingia Marekani kwa njia zisizo halali wakiwa watoto kuishi nchini humo.

USA Daca-Programm Proteste in in Oklahoma City
Picha: picture-alliance/AP Photo/

Mwanasheria Mkuu wa Marekani Jeff Sessions ameutaja mpango huo wa kuahirisha hatua kuchukuliwa dhidi ya watoto hao ujulikanao DACA kuwa kinyume na katiba akiongeza kuwa utawala wa Trump umeaumua kuusitisha mpango huo.

Mpango huo wa DACA ulianzishwa na aliyekuwa Rais wa Marekani Barack Obama miaka mitano iliyopita ili kuwalinda vijana hao dhidi ya kurejeshwa makwao na kuruhusiwa kusoma na kufanya kazi Marekani.

Obama ambaye aliahidi kutoingilia masuala ya kisiasa baada ya kustaafu ametoa taarifa akiushutumu uamuzi huo wa Trump kwa kuutaja usio sahihi, wa kinyama na unaowaadhibu wasio na hatia.

Trump asema Wamarekani kwanza

Trump amejitetea akisema ni muhimu kulinda sheria za nchi akiongeza hapendi kuwaadhibu watoto ambao wengi wao sasa hivi ni watu wazima lakini kuna haja ya kutambua umuhimu wa kuheshimu sheria na kuchukua hatua kudhibiti sheria za uhamiaji ili kutoa fursa  kwa Wamarekani kwanza.

Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Getty Images/AFP/N. Kamm

Hatua hiyo ya serikali ya Trump imeshutumiwa vikali na pande zote mbili za kisiasa nchini humo kwa kuweka mustakabali wa siku za usoni wa vijana hao katika hali ya mashaka.

Viongozi wa upinzani Democrats, wa kibiashara, asasi za kiraia, makundi ya kidini, na hata wanasiasa wengi wa chama cha Republican wameshutumu kufutiliwa mbali kwa mpango wa DACA  uliokuwa ukiwalinda wahamiaji walioingia Marekani wakiwa chini ya umri wa miaka 16.

Ivan Ceja mwanaharakati wa kutetea haki za wahamiaji ambaye aliwasili Marekani akiwa mtoto mchanga amesema wahamiaji wanaojulikana Dreamers wengi wao kutoka nchi za Amerika kusini walio sasa katika miaka ya ishirini watakuwa na kati ya miezi sita na miezi 24 kabla ya kutajwa kuwa wahamiaji haramu na kuwa katika hatari ya kurejeshwa katika nchi walizotokea.

Bunge latwisha jukumu la kufanya mageuzi

Trump amesisitiza kuwa anawapenda wahamiaji hao na kulitaka bunge kupitisha mageuzi makubwa kuhusu sheria za uhamiaji, jambo ambalo wabunge wa Marekani wamejaribu na kushindwa kwa miongo kadhaa. Rais huyo wa Marekani ameaahidi kulitathmini tena suala hilo iwao bunge litashindwa.

Waandamanaji wakipinga kufutiliwa mpango wa DACAPicha: picture-alliance/abaca/O.Douliery

Seneta wa Republican John McCain amesema licha ya kuwa alitofautiana na Obama kuhusu kutumia mamlaka yake kama rais kuidhinisha mpango huo, kuubatilisha wakati huu ni jambo lisilokubalika na ameapa kushirikiana na Wademocrats na wanasiasa wenzake wa Republican kupitisha mageuzi makubwa ya uhamiaji bungeni.

Baraza la maaskofu wa Kanisa Katoliki la Marekani limeutaja uamuzi wa Trump kinyume na jinsi maandiko yanavyotaka viongozi kuwalinda wasiobahatika katika jamii.

Mwandishi: Caro Robi/afp

Mhariri: Bruce Amani