1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump awasili Qatar, atangaza mkataba mnono na Boeing

14 Mei 2025

Rais wa Marekani Donald Trump aliwasili mjini Doha Jumatano, katika kituo cha pili cha ziara yake ya siku kadhaa Mashariki ya Kati, na kupokelewa kwa heshima kubwa na Emir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani.

Qatar Doha 2025 | Emir Al-Thani ampokea Rais Trump uwanja wa ndege
Emir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, akimkaribisha Rais Donald Trump katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Hamad.Picha: Qatar News Agency/IMAGO

Akiwa Doha, Trump alitangaza kutiwa saini kwa mkataba wa kihistoria kati ya Shirika la Ndege la Qatar Airways na kampuni ya Marekani ya Boeing, wenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 200. Mkataba huo unajumuisha oda ya ndege 160, ambayo Trump alisema ni "oda kubwa zaidi ya ndege kuwahi kupokelewa na Boeing katika historia yake.”

"Ni zaidi ya dola bilioni 200, lakini ndege ni 160. Hii ni rekodi,” alisema Trump mbele ya waandishi wa habari, huku akimpongeza Afisa Mtendaji Mkuu wa Boeing, Kelly Ortberg. "Toeni ndege hizo, zifike kule nje haraka,” aliongeza kwa msisitizo.

Dili hiyo ya anga ilitiwa saini mbele ya Trump na Emir wa Qatar katika jumba la kifalme la Amiri Diwan, ikiwa ni sehemu ya mikataba kadhaa ya kiuchumi inayolenga kukuza ushirikiano wa kibiashara kati ya Doha na Washington. Ingawa haikubainika mara moja aina ya ndege zitakazojumuishwa, wachambuzi wa masuala ya anga wamesema ni kawaida kwa Boeing kutoa punguzo kubwa kwa oda za wingi.

Soma pia: Trump akutana na Rais mpya wa Syria katika mabadiliko makubwa ya kidiplomasia

Trump aliwasili Qatar akitokea Riyadh, Saudi Arabia, ambako aliweka historia kwa kukutana na Rais wa mpito wa Syria, Ahmed al-Sharaa, na kutangaza kuondolewa kwa vikwazo vyote vya kiuchumi dhidi ya taifa hilo. Hatua hiyo ilielezwa na wachambuzi kama mabadiliko makubwa ya sera ya Marekani kuelekea Syria.

Trump aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hamad mjini Doha, huku uhusiano kati ya serikali hizo mbili ukiwa katika mjadala kufuatia ofa ya Qatar kumpa Trump ndege ya kifahari yenye thamani ya dola milioni 400, ambayo ingeanza kutumika kama Air Force One na baadaye kuhamishiwa kwa matumizi yake binafsi.Picha: Brendan Smialowski/AFP

"Vikwazo hivyo vilikuwa vinakandamiza sana na vyenye nguvu kubwa. Haitakuwa rahisi hata hivyo, lakini hii inawapa nafasi nzuri na thabiti ya kuanza upya,” alisema Trump katika hotuba yake kwa viongozi wa Ghuba, akisisitiza kuwa uamuzi huo ni fursa kwa Syria kujiimarisha kiuchumi na kijamii baada ya miaka ya vita.

Trump aitaka Syria kurekebisha uhusiano na Israel

Katika mkutano huo, Trump aliongozana na Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, huku Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan akihudhuria kwa njia ya video. Licha ya upinzani kutoka kwa baadhi ya maafisa wa Israel, Trump alisema al-Sharaa ameonesha nia ya kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na Israel kupitia makubaliano ya Abrahamu.

Alipoulizwa na waandishi wa habari iwapo safari yake ya Mashariki ya Kati inamaanisha kuipuuza Israel, Trump alijibu: "Hapana kabisa. Hii ni nzuri kwa Israel. Kuwa na uhusiano kama nilio nao na nchi hizi za Kiarabu—nafikiri ni faida kubwa kwa Israel.”

Wakati huo huo, Trump alizungumzia suala la Iran na mazungumzo ya nyuklia yanayoendelea, akisisitiza kuwa yuko tayari kufanya makubaliano ikiwa Tehran itaacha kufadhili makundi ya wapiganaji wa uwakili kama Hamas, Hezbollah, na Wahouthi. "Iran lazima isitishe kabisa mpango wake wa kutengeneza silaha za nyuklia. Hawawezi kuwa na silaha hizo,” alisisitiza Trump.

Rais Donald Trump na Emir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani wakihudhuria hafla ya utiaji saini katika Jumba la Amiri Diwan mjini Doha, Qatar, Jumatano, Mei 14, 2025.Picha: Alex Brandon/AP Photo/picture alliance

Soma pia: Trump atangaza kuiondolea vikwazo Syria katika mabadiliko makubwa ya sera ya Washington

Katika hotuba kwa viongozi wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba (GCC), Trump alisisitiza umuhimu wa kupatikana kwa suluhu ya kudumu kuhusu Iran. "Nataka tufikie makubaliano, lakini ikiwa hawatakubali masharti, basi italazimika iwe kwa njia isiyopendeza,” alisema, akionya juu ya hatua mbadala ikiwa mazungumzo yatakwama.

Trump pia aliashiria uwezekano wa kuhudhuria mazungumzo ya amani kati ya Urusi na Ukraine, yanayotarajiwa kufanyika Alhamisi mjini Istanbul. "Nikiwa pale, kuna uwezekano mkubwa Putin naye atafika. Kama tunaweza kumaliza vita, nitafikiria kwenda,” alisema Trump akiwa ndani ya ndege ya Air Force One kuelekea Doha.

Ziara ya Trump nchini Qatar inachukuliwa kama jaribio la kuimarisha ushawishi wa Marekani katika eneo hilo, sambamba na kufungua ukurasa mpya wa uhusiano na serikali mpya ya Syria. Trump anatarajiwa kuendelea na ziara yake kwa kutembelea Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kabla ya kurejea Washington.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW