1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump: 'Hatutathibitisha makubaliano ya nyuklia na Iran'

Yusra Buwayhid
14 Oktoba 2017

Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza uwezekano wa kuiondoa nchi yake katika makubaliano ya kimataifa yaliyopelekea Iran kuondolewa vikwazo vya kibiashara kwa kukubali kusitisha mpango wake wa nyuklia.

USA PK Präsident Trump über Atomabkommen mit Iran
Picha: Reuters/K. Lamarque

Rais huyo wa Marekani ameuhimiza ulimwengu kuishinikiza Iran kukomesha kile alichokiita "harakati zitakazo sababisha vifo na uharibifu." Trump alisema Iran imefanya ukiukwaji wa mkataba huo na kutoa wito wa kukiwekea vikwazo kikosi maalumu cha jeshi la Iran kinachojulikana kama Walinzi wa Mapinduzi.

"Leo hii ninatangaza mkakati wetu pamoja na hatua kadhaa tutakazozichukua kuhakikisha Iran kamwe na  ninamaanisha kamwe haitengenezi silaha za nyuklia. Kuna haja gani ya kuwa na makubaliano ambayo uwezo wake mkubwa ni kuchelewesha tu mpango wa nyuklia wa Iran  kwa muda mfupi?", alisema Trump katika hotuba yake siku ya Ijumaa.

Baada ya hotuba ya Trump, rais wa Iran Hassan Rouhani alisema ikiwa maslahi ya nchi yake yataendelea kulindwa, Iran itaendelea kutimiza matakwa ya makubaliano hayo.

Trump hata hivyo hakuchukua uamuzi wa moja kwa moja, badala yake ameliachia Bunge la Congress kufanya maamuzi ya mwisho. Wabunge wana siku 60 za kuamua kama wanataka kuiwekea tena vikwazo vya kibiashara Iran. Hata hivyo, hawalazimiki kisheria kufanya hivyo, wanaweza kuziachilia siku hizo 60 kupita bila ya kuchukua uamuzi wowote.

Rais Donald Trump akitoa masimamo wake kuhusu makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na mataifa makubwa sita, ambayo amesema hayana uthibitisho wake.Picha: Reuters/K. Lamarque

Umoja wa Ulaya watoa msimamo

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini alisema makubaliano yanayohusu mpango wa nyuklia wa Iran ni madhubuti na yanafanya kazi vizuri na kuongeza kuwa hayawezi kusambaratishwa na kiongozi yeyote, akiwamo rais wa Marekani Donald Trump.  Mogherini ndiye alikuwa mpatanishi rasmi wa Umoja wa Ulaya katika makubaliano hayo yaliohitimishwa mwaka 2015.

"Mkataba huo siyo makubaliano kati ya mataifa mawili, huu siyo mkataba wa kimataifa, lakini ni sehemu ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa," alisema Mogherini baada ya tangazo la Trump, "hivyo haiko katika mamlaka ya rais yeyote wa taifa lolote duniani kuvunja mkataba wa aina hii."

"Rais wa Marekani ana mamlaka makubwa, lakini siyo juu ya mkataba huu," aliongeza mkuu huyo wa sera ya kigeni wa Umoja wa Ulaya.

Mogherini pamoja na  maafisa wengine wa Umoja wa Ulaya wanasisitiza kuwa wataendelea kuheshimu makubaliano hayo, na kuikumbusha Iran kuwa inapaswa kufanya hivyo pia. Taarifa ya pamoja ya serikali za Ufaransa, Ujerumani na Uingereza ilimsihi Trump kutafakari upya hatua zake.

Matatizo mengine yatofautishwe na mkataba wa nyuklia

Afisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya akizungumza kabla ya tangazo hilo, alisema kanda hiyo inakubaliana na Trump kuhusu hatari za makombora ya masafa marefu, ugaidi, wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran na kile wanachokiona kama tabia mbaya, na kwamba wanaamini hayo yanapaswa kushughulikiwa, lakini kwa kutofautishwa na mkataba wa nyuklia.

Rais wa Iran Hassan Rouhani asema ikiwa maslahi ya nchi yatalindwa atakuwa tayari kuheshimu makubaliano.Picha: picture alliance/AP Photo/Iranian Presidency Office

Alau kwa mkataba wa sasa wa nyuklia, Tehran haitokuwa na vichwa vya nyuklia vya kuweka kwenye makombora hayo, alisema afisa huyo. Sasa zingatio la ushawishi linaelekezwa lwa bunge la Marekani, ambako juhudi za Ulaya zinaendelea, kwa mujibu wa afisa huyo.

"Masuala yote mengine muhimu yanayoweza kujitokeza hayatoweza kushughulikiwa ikiwa tutavunja mkataba huu," alisema afisa huyo, " kwa sababu makubaliano hayo yanaondoa hatari kubwa sana, siyo tu hatari ya mashindano ya kuunda silaha za nyuklia katika kanda hiyo, lakini pia kuenea kwa nyuklia kusikodhibitiwa, jambo ambalo kwa bahati mbya tunalishuhudia nchini Korea Kaskazini."

Ukosefu wa maafikiano kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya

Mchambuzi kutoka Baraza la Ulaya la Uhusiano wa Kigeni Ellie Geranmayeh, amesema hatua hii "imetazamwa barani Ulaya kama usaliti mbaya wa washirika wa Ulaya." Wakati Waulaya wana wasiwasi pia kuhusu kuenea kwa makombora na uingiliaji wa Iran katika mataifa ya kikanda, wanataka kuendeleza njia za kidiplomasia.

 "Ikiwa mkataba huu utaanza kuvunjika," aliiambia DW, kuna uwezekano mkubwa wa kuchochea shughuli kutoka kwa Iran ndani ya kanda, ambazo zitaongezea hali tete katika kanda hiyo.

Erik Brattberg, anaeongoza programu ya Ulaya Wakfu wa Carnegie, anasema kwamba ingawa hisia za Umoja wa Ulaya ni za kuvunjwa moyo, hali hiyo haihitaji kuonekana kama "janga."

"Wakati mashaka kuhusu nia ya Marekani na dhamira yake kwa makubaliano hayo vinaonekana kutoepukika katika kipindi cha muda mfupi," Brattberg alisema, "inapendelewa angalau kuliko kujitoa kikamilifu kwa Marekani kutoka mkataba huo katika mtazamo wa Ulaya.

Mkuu wa sera ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini amesema hakuna rais yeyote anaeweza kufuta makubaliano ya nyuklia na Iran kivyake.Picha: Reuters/E. Vidal

Vikwazo dhidi ya Iran vinaweza pia kuiumiza EU

Lakini mambo yatakuwa mabaya kwa makampuni ya Umoja wa Ulaya ambayo yameanzisha tena biashara ya Iran iwapo shauku ya Trump itatimizwa. "Nadhani kuna nafasi kubwa kwamba vikwazo vya Marekani vitarejeshwa dhidi ya Tehran," anatabiri Nile Gardiner, Mkurugenzi wa Kituo cha Uhuru cha Margaret Thatcher katika  Wakfu wa Heritage, ambao ni shirika la ushauri la kihafidhina mjini Washington.

Warepublican wataunga mkono kwa nguvu kurejeshwa vikwazo, alisema, na baadhi ya Wademocrat wanaweza kuungana nao.

Kampuni za Ulaya zinapasw akuwa na wasiwasi," Gardiner aliiambia DW. " Wanacheza na moto kwa kuwekeza nchini Iran, na wanaweza kukumbwa kuumizwa vibaya na vikwazo vya Marekani. Ikiwa wanataka kufanya biashara na Marekani watalaazimika kuheshimu vikwazo vya Marekani iwapo vitawekwa."

Geranmayeh anaona kuwa huenda Gardiner akawa sahihi. "Ujumbe wangu kwa Waulaya ni, kwa vile sasa Trump ameondoa uthibitisho, bora muanze kufikiria mipango ya dharura kwa kasi kuliko hapo kabla," alisema, iwe kwa sababu ya mchakato wa kutathmini upya wa Congress au kwa sababu, ifikapo Januari, rais anaamua kuvunja mkataba huo."

Mnamo wakati mawaziri wa mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya wakikutana siku ya Jumatatu kujadili mkakati wao, Geranmayeh anasema hata ikiwa Umoja wa Ulaya umeungana katika msimamo mmoja wa kuendelea na makubaliano hayo, wanapaswa kuanza kupanga juu ya umbali gani wako tayari kufika katika kuokoa makubaliano hayo na namna ya kuyalinda makampuni yao dhidi ya Ikulu ya White House ikiwa yote yatashindwa.

Shada Islam, mkurugenzi wa sera katika taasisi ya Freinds of Europe, alitikisa tu kichwa kuhusu matukio hayo. "Huu ni mkataba uliopiganiwa kwa nguvu zote," aliiambia DW, na kuongeza kuwa kuufuta kutasababisha hatari kwa dunia. "Hii itawawezesha wale wote wasiopenda mktaba wa nyuklia nchini Iran - hilo ndiyo tunataka?"

Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amesema uamuzi wa Rais Trump ni hatari kwa ulimwengu.Picha: Reuters/A.Brandon

John Kerry: Ni uamuzi wa hatari

Waziri wa zamani wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry, mmoja wa waliofanya juhudu kubwa kufanikisha makubaliano hayo, amesema Rais Trump anatengeneza mgogoro wa kimataifa kwa uamuzi wake wa hatari wa kuondoa uthibitisho juu ya mkataba huo.

"Unahatarisha maslahi ya usalama wa taifa la Marekani na wa washirika wetu wa karibu," alisema Kerry na kulitolea mwito bunge kumzuwia Trump. "Hiyo inamaanisha kuukata mpango wa rais na ujanja unaotafakariwa bungeni ambao utapelekea mktaba huo kuvunjika mara moja.

Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya miaka kadhaa ya mazungumzo. Mkataba huo wa kimataifa uliotiwa saini mwaka 2015 ni alama ya ushindi mkubwa wa mazungumzo ya kidiplomasia kwa nchi zilizoshiriki, ikiwa ni pamoja na Ujerumani, China, Ufaransa, Urusi, Uingereza, Umoja wa Ulaya na Marekani, zilizoitaka Iran kupunguza uwezo wake wa kutengeneza silaha za kinyuklia ili iweze kuondolewa vikwazo ilivyokuwa imewekewa.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/ap/dw

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW