1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump kuapishwa kuwa Rais wa 47 wa Marekani

20 Januari 2025

Rais mteule wa Marekani, Donald Trump, anatarajiwa kuapishwa Jumatatu kuiongoza nchi hiyo, huku akirejea katika Ikulu ya Marekani, White House kwa muhula wa pili wa miaka minne.

Rais mteule wa Marekani, Donald Trump
Rais mteule wa Marekani, Donald TrumpPicha: Scott Olson/Getty Images

Katika sherehe hizo zinazofanyika mjini Washington majira ya saa tano na nusu asubuhi kwa saa za Marekani, Trump, mwanachama wa chama cha Republican, anachukua nafasi ya Rais anayeondoka madarakani Joe Biden, baada ya kumshinda Makamu wa Rais anayemaliza muda wake Kamala Harris katika uchaguzi wa urais uliofanyika mwezi Novemba mwaka 2024.

Trump kuhudhuria Ibada ya Misa kabla ya kuapishwa

Kulingana na Kamati ya sherehe za Kuapishwa Trump, rais huyo mteule wa Marekani, atakula kiapo mbele ya Jaji Mkuu John Roberts. Kamati hiyo imesema asubuhi Trump amepangiwa kuhudhuria Ibada ya Misa katika Kanisa la Mtakatifu John mjini Washington.

Rais wa Marekani anayemaliza muda wake Joe BidenPicha: Stephanie Scarbrough/AP/picture alliance

Baada ya kula kiapo cha kuiongoza Marekani, Trump atahutubia kwa mara ya kwanza kama Rais wa 47 wa Marekani. Na baada ya hapo Biden na Mkewe, Jill, watamkaribisha Trump na mkewe Melania, kwa dhifa ya chai na kahawa katika Ikulu ya White House.

Awali sherehe za kuapishwa Trump, mwenye umri wa miaka 78 zilikuwa zifanyike kama kawaida nje ya Majengo ya Bunge upande wa magharibi, lakini zikahamishiwa ndani kutokana na hali ya hewa ya Washington ambayo viwango vya nyuzi joto ni chini ya sifuri.

Makamu mteule wa Rais wa Marekani JD Vance, anatarajiwa kuapishwa na Jaji wa Mahakama ya Juu, Brett Kavanaugh.

Trump aapa kushughulikia mizozo ya Marekani

Hata hivyo, katika mkutano maalum wa kabla ya kuapishwa kwake uliofanyika jana Jumapili mjini Washington, Trump aliwaambia wafuasi wake kwamba mara atakaoipingia katika Ikulu ya White House, atahakikisha anaushughulikia kila mzozo unaolikabili taifa hilo na kupitisha amri kadhaa za kiutendaji, na kubatilisha hatua nyingi zilizowekwa na rais anayeondoka madarakani Joe Biden.

"Ndani ya saa chache baada ya kuchukua madaraka, nitasaini amri kadhaa za kiutendaji, takribani 100, ambazo nyingi nitazieleza katika hotiba yangu kesho. Hatutapoteza hata dakika moja katika kutekeleza ahadi zetu kwa wananchi," alifafanua Trump.

Maelfu ya wafuasi wa Donald TrumpPicha: Celal Gunes/Anadolu/picture alliance

Trump amesema ataanza pia mara moja kuwarudisha makwao wahamiaji wasio na vibali maalum. Katika mkutano huo uliohudhuria na umati mkubwa wa watu, Trump alisema atazuia uvamizi katika mipaka ya Marekani, na kubadili sera ikiwa ni pamoja na suala la watu wanaobadili jinsia katika shule za Marekani.

Historia ya kuingia, kutoka na kurejea tena White House

Trump anaweka historia kwa kuwa rais mwenye umri mkubwa kuapishwa. Pia Trump ameingia katika historia ya Marekani kwa kuwa rais wa pili kuongoza kwa muhula mmoja kama rais, kuondoka madarakani na kisha kurejea tena katika Ikulu ya White House. Rais wa kwanza alikuwa Grover Cleveland mwaka 1893.

Ushindi wa Trump ulipongezwa na kuwatia moyo wanasiasa wanaofuata siasa za mrengo wa kulia ulimwenguni. Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni, mwanachama wa siasa kali za mrengo wa kulia, atahudhuria uapisho wa Trump na tayari amewashawasili mjini Washington.

(DPA, AFP, AP)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW