1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump kuiadhibu vikali Saudia kutokana na kupotea Khashoggi

13 Oktoba 2018

Rais wa Marekani, Donald Trump amesema Saudi Arabia huenda ikawa inahusika na kutoweka kwa mwandishi habari wa Saudia, Jamal Khasshogi na ameonya kuwa Marekani itachukua hatua kali iwapo mwandishi huyo ameuawa.

Donald Trump Mohammed bin Salman Saudi Arabien
Picha: picture alliance/dpa/M.Wilson

Khashoggi mkosoaji mkubwa wa serikali ya Saudi Arabia hajaonekana tangu alipoingia kwenye ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul, Uturuki, Oktoba 2, huku maafisa wa Uturuki wakiishutumu Saudi Arabia kwa kumuua mwandishi huyo ndani ya ubalozi.

Akizungumza katika kipindi cha ''Dakika 60'' cha kituo cha televisheni cha CBS, Trump amesema wanafanya uchunguzi wa kina kuhusu kutoweka kwa Khashoggi ili kupata ukweli na watatoa adhabu kali. Amesema Marekani itasikitika sana na kuchukizwa wakigundua kuwa Saudia inahusika.

''Hadi sasa, wamekana na wamekataa kabisa. Je inaweza ikawa wao? Ndiyo, amesema Trump katika mahojiano hayo yaliyofanyika siku ya Alhamisi na kurushwa leo Jumamosi. Trump aliyajibu hayo baada ya kuulizwa iwapo Khashoggi aliuawa na Saudi Arabia.

Jamal KhashoggiPicha: picture-alliance/AP Photo/V. Mayo

Kituo hicho cha CBS kimesema kitayarusha mahojiano yote Jumapili ya Oktoba 14. Trump ameongeza kusema kuwa suala hilo ni muhimu sana kwa sababu mtu huyo alikuwa mwandishi habari. Lakini alipoulizwa kuhusu hatua anayoweza kuchukua, Trump alisema hakuwa na nia ya kuzuia mauzo ya silaha katika taifa hilo la Kifalme, msimamo aliokuwa nao awali.

Amesema hataki kuharibu ajira za watu na hataki kuikosa hiyo biashara kwa sababu kila mtu duniani anaitaka, ikiwemo Urusi na China na amebainisha kwamba kuna njia nyingi za kuiadhibu Saudi Arabia. Hata hivyo, Saudi Arabia leo imekanusha kuhusika na madai kwamba waliamuru mauaji ya Khashoggi, wakiyaelezea kuwa ni ya ''uongo na yasiyo na msingi''.

Hayo yanajiri wakati ambapo Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu akiitaka Saudi Arabia kutoa ushirikiano katika uchunguzi wa kutoweka kwa Khashoggi. Cavusoglu alikuwa akizungumza na waandishi habari wakati wa ziara yake mjini London, Uingereza, siku moja baada ya ujumbe wa Saudia kuwasili Uturuki kwa ajili ya uchunguzi wa kisa hicho. Ameitaka Saudia kuwaruhusu maafisa wa Uturuki kuingia katika ubalozi wake mdogo mjini Istanbul.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio GuterresPicha: picture-alliance/AP Images/R. Drew

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema wanahitaji kufahamu kilichotokea hasa na nani anahusika. Guterres amesema ana wasiwasi kuhusu sakata hili na kwamba ukweli unapaswa kujulikana wazi. Kwa upande wake Mkuu wa Shirika la Fedha Duniani, IMF, Christine Lagarde amesema ana hofu kuhusu hatma ya Khashoggi, lakini ana mipango ya kuhudhuria mkutano wa kiuchumi utakaofanyika mjini Riyadh baadae mwezi huu.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, DPA, Reuters
Mwandishi: Yusra Buwayhid

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW