Trump kuitumia Japan katika mazungumzo na Iran
27 Mei 2019Trump ambaye alisema ana nia ya kufanya mazungumzo na Iran, alikuwa akitumai kupunguza hofu ya mzozo wa kijeshi lakini Iran imesema haina haja ya kuwaisliana na Ikulu ya White House. Trump amesema anafahamu uhusiano mzuri uliopo baina ya Japan na Iran na anatazamia kumuunga mkono waziri mkuu Abe.
"Naamini Iran wako tayari kuzungumza na kama wanataka kuzungumza, sisi pia tungependa hivyo, lakini najua ukweli kwamba waziri mkuu Abe ana uhusiano wa karibu na uongozi wa Iran. Tutaona nini kitakachotokea na itakuwa sawa. Hakuna mtu anayependa kuona mambo mabaya yanatokea hususan mimi", alisema Trump.
Abe anakusudia kuitembelea Iran mwezi ujao katikati ya mzozo unaozidi kutokota baina ya nchi hiyo na Marekani juu ya mpango wa nyuklia wa Iran.
Trump ameiwekea vikwazo vikali Iran ambavyo vinauathiri uchumi wake. Mwishoni mwa wiki iliyopita, alitangaza kuongeza wanajeshi 1500 katika ukanda huo mnamo wakati mvutano ukiendelea kuongezeka. Pia Marekani ilipeleka ndege za kivita katika Ghuba ya Uajemi katika kukabiliana na kile inachodai ni kitisho kutoka kwa Iran.
Kabla ya mazungumzo yake na Abe, rais Trump alikutana na Mfalme mpya Naruhito na kumfanya kuwa kiongozi wa kwanza wa dunia kukutana na kiongozi huyo baada ya kutawazwa Mei mosi.
"Ilikuwa heshima kubwa kwetu kukaribisha wewe katika uongozi mpya wa Kifalme Reiwa", alisema Abe.
Trump alisalimiana na Mfalme Naruhito na Malkia Masako. Mbali na mvutano na Iran, pia suala la Korea Kaskazini na biashara ni ajenda zilizogubika mazungumzo ya Trump na Abe. Kwa mujibu wa Trump, hadi kufikia mwezi Agosti nchi hizo mbili zitatangaza mambo mazuri kwa ajili ya nchi hizo mbili.
Trump anadai kuwa Japan "imekuwa ikifanya biashara zaidi na Marekani" na kwamba nchi yake inataka sasa nayo ifaidike na biashara zaidi na Japan. Kuhusu Korea Kaskazini, Trump amesema anayo matumaini kwamba mzozo wao utapatiwa ufumbuzi. Korea Kaskazini imemuita mshauri wa usalama wa Trump John Bolton kuwa "mchuuzi wa vita", baada ya wiki iliyopita kutoa kauli akisema majaribio ya makombora yaliyofanywa na Korea Kaskazini mnamo Mei 4 yalikiuka maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.