Trump kuiuzia Nigeria ndege za kivita
11 Aprili 2017Bunge la Marekani linatarajiwa kupokea taarifa rasmi wiki chache zijazo, na kuanzisha mchakato wa mpango huo na Nigeria ambao utawala wa Obama ulikuwa umepanga kuuidhinisha mwishoni kabisa mwa muhula wake.
Mpango huo utaiwezesha Nigeria kununua ndege 12 aina ya Embraer A29 Super Tucano ambazo zina vifaa vya kisasa kabisa, zitakazogharimu dola milioni 600. Ijapokuwa Rais Donald Trump amesema wazi nia yake ya kuidhinisha mauzo ya ndege hizo, Baraza la Usalama wa Taifa bado linalifanyia kazi suala hilo. Nigeria imekuwa ikitaka kununua ndege hizo za kivita tangu mwaka wa 2015.
Jeshi la Nigeria linatuhumiwa kuyalipua makaazi ya raia karibu mara tatu katika miaka ya karibuni. Katika tukio baya zaidi, ndege ya kivita mnamo Januari 17 iliilipua kambi moja ya eneo la Rann, karibu na mpaka na Cameroon, ambako raia walikuwa wamechukua hifadhi kutokana na mashambulizi ya Boko Haram. Kati ya raia 100 na 236 na wafanyakazi wa misaada waliuawa, kwa mujibu wa takwimu za maafisa na vingozi wa kijamii.
Ulipuaji huo ulifanyika mnamo siku ambayo utawala wa Obama ulinuia kulifahamisha rasmi Bunge kuwa utasonga mbele na mpango huo wa mauzo. Badala yake, ulisitishwa kwa ghafla, na siku chache baadaye, Trump akaapishwa.
Shirika la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International linalituhumu jeshi la Nigeria kufanya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadaamu katika mauajo ya kiholela ya karibu washukiwa 8,000 wa Boko Haram.
Rais Muhammadu Buhari aliahidi kuchunguza madai hayo ya ukiukaji baada ya kuingia madarakani mwaka wa 2015, lakini hakuna mwanajeshi yeyote aliyeshitakiwa na maelfu ya watu bado wanazuiliwa kinyume cha sheria katika vituo vya kijeshi. Jeshi la Nigeria linakanusha madai hayo.
Nigeria pia iko ukingoni mwa eneo la Sahel, ambalo ni jangwa linalounganisha Sahara Kaskazini na Kusini ambako watalaamu wanaonya kuwa wanamgambo wa itikadi kali kama vile Boko Haram huenda wakapanua udhibiti wao.
Mpango huo wa ndege pia ungeweza kuyaridhisha malengo ya Trump ya kuyaunga mkono mataifa yanayopambana dhidi ya ugaidi, kuimarisha viwanda vya Marekani na kutengeneza nafasi za mishahara ya juu nchini Marekani.
Mara baada ya Bunge kufahamishwa kuhusu mauzo hayo, wabunge wanaotaka kuupinga mpango huo wana siku 30 kupitisha sheria isiyoweza kupingwa kupitia kura ya turufu.
Ndege za A-29, ambazo usiku huwawezesha marubani kulenga shabaha maeneo ya kulipua, zinatengenezwa mjini Jacksonville, jimboni Florida.
Mwandishi: Bruce Amani/AP
Mhariri: Oummilkheir