1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump kujiondoa mkataba wa Iran

6 Oktoba 2017

Rais wa Marekani, Donald Trump anapanga kujiondoa katika mkataba wa nyuklia na Iran katika tangazo analopanga kulitoa wiki ijayo, kabla ya muda wa mwisho uliowekwa wa kutolewa ripoti iwapo Iran inauzingatia mkataba huo.

Donald Trump Treffen mit Militärführung
Picha: Reuters/Y.Gripas

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa jana na vyombo vya habari vya Marekani, Trump amesisitiza kwamba Iran haijafanya vya kutosha katika kuuzingatia mkataba huo wa kimataifa na kusitisha mpango wake wa nyuklia. Akizungumza jana na viongozi wa kijeshi, Trump amesema mambo yanayofanywa na Iran hayaendani na makubaliano ya mkataba huo.

''Hatupaswi kuiruhusu Iran ifanikiwe kutengeneza silaha za nyuklia. Utawala wa Iran unaunga mkono ugaidi na umekuwa ukieneza ghasia na machafuko kuzunguka eneo la Mashariki ya Kati, ndiyo maana lazima tukomeshe uchokozi huu unaoendelea kufanywa na Iran katika mpango wake wa nyuklia. Lazima wazingatie yaliyoandikwa kwenye mkataba,'' alisema Trump

Kinu cha nishati ya nyuklia cha IranPicha: picture-alliance/dpa/A. Taherkenareh

Kwa mujibu wa taarifa, Trump atasema kuwa mkataba wa Iran uliofikiwa mwaka 2015 baada ya miaka kadhaa ya mazungumzo kati ya Iran na mataifa sita yenye nguvu duniani, hauna maslahi kwa taifa la Marekani. Trump anapaswa kuliambia baraza la Congress la Marekani, iwapo anaamini Iran inayafuata makubaliano hayo au la, ifikapo Oktoba 15.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Sarah Sanders amesema Trump ameshafanya maamuzi kuhusu mkataba wa Iran na atatoa kauli yake katika muda muafaka. Maafisa wa Ikulu ya Marekani wameonya dhidi ya taarifa zinazoenezwa kwamba Trump atahutubia kuelezea uamuzi wake, Alhamisi ijayo.

Marekani imejiingiza kwenye mkataba mbaya

Wakati wa kampeni za uchaguzi wa urais wa Marekani mwaka uliopita, Trump alilalamika kwa uchungu kuhusu mkataba wa Iran na katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa uliofanyika mwezi uliopita, Trump aliuita mkataba huo kama 'mmoja kati ya mikataba mibaya kabisa' ambayo Marekani imejiingiza.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei LavrovPicha: picture alliance/TASS/dpa/A. Shcherbak

Hata hivyo washauri wa ngazi ya juu wa kijeshi wa Trump, akiwemo Waziri wa Ulinzi, James Mattis na Mwenyekiti wa baraza la uongozi wa majeshi ya Marekani, Jenerali Joseph Dunford wameelezea hadharani kwamba wanauunga mkono mkataba huo wa Iran.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov amesema leo kuwa ana matumaini Rais Trump atatoa uamuzi sawia uwiano kuhusu mkataba huo wa kimataifa wa nyuklia wa Iran. Amesema ni muhimu kuuwacha kama ulivyo sasa na ushiriki wa Marekani utakuwa muhimu sana. Lavrov ameyasema hayo mbele ya waandishi habari akiwa nchini Kazakhstan.

Kulingana na mkataba huo, Iran ilikubali kuzuia mpango wake wa nyuklia ili iweze kuondolewa vikwazo vya kimataifa ambavyo vimesababisha uchumi wa nchi hiyo kuyumba.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, DPA, Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman