Trump kujisalimisha jimboni Georgia katika kesi ya uchaguzi
22 Agosti 2023Kupitia mtandao wake wa kijamii wa Truth Social siku ya Jumatatu, Trump alisema kwamba siku hiyo ya Alhamis "atakamatwa na Mwanasheria mwenye misimamo mikali, Fani Wills" ambaye alifungua mashitaka ya nne katika mwaka huu dhidi ya rais huyo wa zamani. Jaji katika kesi hiyo, awali aliidhinisha dhamana ya Dola za Kimarekani laki 200,000 kwa Trump katika kesi hiyo ya udaganyifu iliyofunguliwa dhidi yake katika jimbo la kusini.
Kuhusu kesi nyingine zinazomkabili Trump: Majaji kumchunguza Trump kwa jaribio la kupindua uchaguzi
Trump na washitakiwa wengine 18 katika kesi hiyo ya kihistoria watakuwa na muda wa mwisho wa hadi saa sita mchana siku ya Ijumaa kujisalimisha wenyewe katika mamlaka za Georgia. Kwenye ujumbe wake kupitia Truth Social, Trump amedai kwamba mwanasheria Wills "anashirikiana na wizara ya sheria ya kihuni ya Joe Biden", akiongeza kuwa inahusiana na uingiliaji uchaguzi. Hiyo ni njia ya Trump kusema kwamba mashitaka yote dhidi yake yamesukwa ili kuzuia jaribio lake la kuwania muhula wa pili wa urais wakati akiongoza ndani ya chama chake cha Republican.
Soma pia: Kesi ya Trump itaanza kusikilizwa Mei 2024
Mbali na dhamana ya dola laki 200,000 kwa bilionea huyo wa Republican, Jaji wa mahakama ya kaunti ya Fulton, Scott McAfee alimwekea masharti kadhaa Trump katika makubaliano yaliyoidhinishwa na waendesha mashitaka na mawakili wake. Miongoni mwa masharti hayo ni lile linalomtaka Trump "kutotafanya kitendo chochote cha kumtisha mtu yeyote anayejulikana kwake kuwa mshtakiwa au shahidi katika kesi hii au kuzuia utoaji wa haki" alisema jaji McAfee katika hati ya mashitaka ya kurasa tatu katika mahakama.
Mwanasheria Wills amemwomba Jaji kupanga tarehe ya kusikilizwa kesi hiyo kuwa Machi 4 hapo mwakani dhidi ya rais huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 77 kwa makosa ya kutaka kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa rais wa 2020 jimboni Georgia. Trump anakabiliwa na mashitaka mengine manne ya jinaiwakati akitafuta kurejea Ikulu ya White House. Mwanasiasa huyo alishitakiwa Georgia kwa tuhuma za udanganyifu na msururu wa uhalifu unaohusiana na uchaguzi baada ya uchunguzi wa miaka miwili juu ya jaribio lake la kutaka kubatilisha matokeo ya ushindi wa Biden katika jimbo hilo. Washitakiwa wengine wanaotuhumiwa kushirikiana na Trump ni pamoja na mwanasheria wake binafsi na aliyekuwa mkuu wa utumishi wa Ikulu Mark Meadows.
Mwendesha maalum Jack Smith amemtaka jaji wa shirikisho kupanga tarehe 2 Januari mwaka 2024 kwa rais huyo wa zamani kufunguliwa mashitaka mjini Washington kwa mashtaka tofauti ya kula njama ya kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa 2020.