Trump kukubaliwa tena kutumia Facebook na Instagram
26 Januari 2023Hii itakuwa imefikisha mwisho hatua ya kuzifunga akaunti hizo kwa kipindi cha miaka miwili kufuatia machafuko yaliyotokea katika majengo ya bunge nchini humo mnamo Januari 6 mwaka uliopita.
Kampuni hiyo ya Meta imesema inaweka "nyenzo mpya za ulinzi" kuhakikisha kwamba hakutokuwa na watu watakaorudia uvunjifu wa sheria zake hata wakiwa wagombea wa kisiasa au viongozi wa dunia.
Makamu wa rais wa masuala ya ulimwengu katika kampuni ya Meta, Nick Clegg, amesema wanachukua hatua hiyo ya kuirudisha tena akaunti ya trump kwa kuwa umma unastahili kusikia wanachokisema wanasiasa wao, kiwe ni kizuri, kibaya au hata cha kutisha ili waweze kufanya maamuzi mazuri wanapokwenda kupiga kura.
Makundi ya kiraia yakosoa kurudishwa kwa akaunti za Trump
Clegg lakini amesema kwamba iwapo kutaonekana hatari yoyote basi kampuni hiyo itaingilia kati. Mkuu huyo wa Meta amesema iwapo Trump atachapisha ujumbe mwengine unaokiuka kanuni za Facebook, basi ujumbe huo utaondolewa na atapigwa marufuku ya kati ya mwezi mmoja na miaka miwili kulingana na kiwango cha ukiukaji huo.
Baada ya kupokea taarifa hiyo ya kufunguliwa tena akaunti yake, Trump ameikosoa Facebook kwa uamuzi wake wa awali wa kuifungia akaunti hiyo huku akiupongeza mtandao wake mpya wa kijamii wa Truth Social.
Makundi ya kiraia yameikosoa hatua hiyo ya kampuni ya Meta yakisema, kumrudisha tena Trump katika Facebook ni ujumbe kwa viongozi wengine walio na ufuasi mkubwa mitandaoni kwamba wanaweza kuvunja sheria bila ya hatua za kudumu kuchukuliwa.
Facebook iliifunga akaunti ya Trump mnamo Januari 7 mwaka 2021 baada ya rais huyo wa zamani kuvisifia vitendo vya vurugu vilivyofanywa na wafuasi wake katika majengo ya bunge ya Marekani, Capitol Hill. Ila kampuni hiyo awali ilikataa miito hata kutoka kwa wafanyakazi wake wenyewe, ya kuiondoa kabisa akaunti ya Trump.
Trump amekuwa akitegemea mtandao wa Truth Social aliouzindua baada ya kufungiwa katika mtandao wa Twitter na mitandao mingine ya kijamii.
Trump alitumia Facebook kuchangisha mamilioni ya fedha za kampeni
Mtandao wa Facebook, sio tu mtandao mkubwa wa kijamii duniani bali ulikuwa ni jukwaa muhimu la Trump kuchangisha mamilioni ya fedha zake za kampeni mwaka 2016 na 2020.
Kurudishwa kwa akaunti hiyo ya Facebook ya Trump ni hatua muhimu kwake kwa kuwa anapanga mikakati ya kuwania urais kwa muhula wa tatu na akaunti hiyo haitompelekea tu kuwasiliana na wafuasi wake milioni 34, bali itatoa fursa kwake aweze kuanza kuchangisha fedha za kampeni tena moja kwa moja.
Wakati akaunti yake ilipofungiwa, wafuasi wake walikuwa wanamchangishia fedha ila hawakuwa na uwezo wa kuweka matangazo ya moja kwa moja kutoka kwake au kwa kutumia sauti yake.
Mitandao mingine ya kijamii kama Snapchat ambapo bado amefungiwa, ilimuondoa katika majukwaa yake baada ya uvamizi huo wa majengo ya bunge. Hivi majuzi akaunti yake ya Twitter ilirudishwa baada ya Elon Musk kuchukua umiliki wa kampuni hiyo ingawa bado nhajaandika ujumbe wowote katika mtandao huo.
Chanzo: AFPE/AP