1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump kupatanisha mgogoro wa Qatar

Sylvia Mwehozi
8 Juni 2017

Rais wa Marekani Donald Trump amejitolea binafsi kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa kidiplomasia unaozidi kutokota katika mataifa ya Ghuba licha ya kuinyoshea kidole Qatar kwamba inafadhili ugaidi.

Auslandreise US-Präsident Trump in Saudi-Arabien
Picha: Getty Images/AFP/M. Ngan

Trump hapo jana amefanya mazungumzo kwa njia ya simu  na Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, akitaka kuisaidia Qatar na mataifa jirani ya kiarabu kupata ufumbuzi wa mgogoro ambao umeuvuruga Umoja wa ukanda wa Ghuba na kupendekeza uwezekano wa kuwepo na mkutano katika Ikulu ya Marekani White House kati ya viongozi.

Ikiwa imetengwa na majirani zake kwa njia ya ardhi na bahari, Qatar iko tayari kukubali msaada wa Trump. Balozi wa Qatar kwa Marekani Meshal bin Hamad al Thani ameliambia shirika la habari la Associated press kuwa nchi yake inaitegemea Washington kuishawishi Saudi Arabia na mataifa mengine kumaliza mzozo huo.

Emir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani Picha: picture-alliance/AP Photo/O. Faisal

Jitihada za Trump za kutaka kusuluhisha mgogoro miongoni mwa serikali za kiarabu kunatofautiana na msimamo wake alioutoa siku moja kabla, ambapo hakuacha hata chembe ya wasiwasi kuhusu nini chanzo cha mzozo huo. Katika tweet yake Trump alisema viongozi wa mashariki ya kati aliokutana  nao mwezi uliopita wote waliionyoshea kidole Qatar kama mfadhili wa ugaidi na kuweka matumaini kwamba kutengwa kwa taifa hilo "kunaweza kuwa ndio mwisho wa hofu ya ugaidi".

Wakati huo huo Amir wa Kuwait amesafiri hadi Qatar akijaribu kusuluhisha mgogoro huo ingawa maafisa wa Falme za Kiarabu wameonya kwamba hakuna cha kusuluhisha.

Amir, Sheikh Sabah Al Ahmad Al Sabah alikutana na mwenzake wa Qatar jana jioni. Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya nje ya Qatar, viongozi hao wawili waligusia namna ya kurejesha mahusiano ya kawaida katika ukanda huo wa Ghuba wakati mwenyeji huyo wa michuano ya kombe la dunia ya 2022 na ktovu cha usafiri wa anga kimataifa likijikuta peke yake baada ya kutengwa ardhini, baharini na angani.

Ndege ya shirika la Qatar Airways Picha: picture-alliance/dpa

Lakini ziara hiyo inakuja baada ya waziri wa mambo ya nje wa Falme za kiarabu Anwar Gargash kusema kwamba Qatar inalipa kile ilichopanda, "hakuna cha kusuluhisha hapa. Kwanza unapaswa kuelewa, kwa mpatanishi yoyote kwamba Qatar inaelewa ukubwa wa tatizo, itikadi kali, ugaidi, na usumbufu na iko tayari kushughulika nao! Kisha rejea makubaliano ya mwaka 2014 na unaangalia masuala mengine katika miaka mitatu iliypita na hapo unaweza kuyaelezea katika namna ambayo unaweza kusema kwamba hivi sasa watatekeleza kile wanachoahidi."

Licha ya juhudi hizo za kutafuta suluhu hali bado inaonekana kuwa tete kwa upande wa Qatar. Shirika la posta la Falme za Kiarabu limesitisha huduma zake zote za posta kwa Qatar, limesema shirika la habari la taifa la WAM hii leo, baada ya mataifa ya kiarabu kukata mahusiano ya kidiploamasia na Qatar mapema wiki hii.

Nazo safari nyingi za  ndege za Qatar airways hivi sasa zinaelekea nchini Iran na Uturuki baada ya kusimamishwa kwingineko Mashariki ya kati.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AP/Reuters

Mhariri: Saumu Yusuf