Trump kupunguza wanajeshi wa Marekani walioko Ujerumani
16 Juni 2020Trump pia ameishutumu Ujerumani akidai haiishughulikii Marekani vyema kibiashara.
Rais Trump amewaambia waandishi wa habari mjini Washington Marekani, kwamba kuna wanajeshi 52,000 wa Marekani walioko Ujerumani na atapunguza idadi hiyo hadi 25,000.
Hata hivyo kulingana na makao makuu ya kijeshi ya Marekani Pentagon, idadi ya wanajeshi iliyotajwa na Trump inapotosha kwa sababu kuna kati ya wanajeshi 34,000 na 35,000 pekee wa kudumu walioko Ujerumani.
Kuondoa wanajeshi ni silaha kuhusu vita vya biashara na Umoja wa Ulaya?
Wanajeshi wa Marekani wamekuwepo Ujerumani tangu mwisho wa Vita Vikuu vya Pili duniani, ambapo walikuwa sehemu kubwa ya wanajeshi wa Jumuia ya Kujihami ya NATO dhidi ya muungano wa Kisovieti wakati wa Vita Baridi.
Kuibuka tena kwa malengo ya kijeshi ya Urusi chini ya Rais Vladimir Putin, kuliipa Marekani umuhimu wa wanajeshi wake kuwepo Ujerumani kwa miongo miwili iliyopita, huku nchi za kati na mashariki mwa Ulaya zikishinikiza kuimarishwa kwa ushirikiano thabiti na Marekani.
Trump amesema anataka kuadhibu kile alichokitaja kuwa mchango usiotosha wa Ujerumani kwa NATO, na kutumia suala la mustakabali wa wanajeshi, kama silaha ya kuunga mkono kitisho chake cha vita vya kibiashara na Umoja wa Ulaya.
Ukosoaji wa mara kwa mara wa Trump dhidi ya washirika katika NATO
Mara kwa mara, Rais Trump amezishutumu nchi wanachama wa NATO kutoka Ulaya, kwa kutotimiza ahadi zao za kutenga angalau asilimia mbili ya mapato jumla ya nchi zao kutumika kwenye ulinzi, badala yake zinategemea Marekani.
Wiki iliyopita, wanasiasa wakuu wa Ujerumani walielezea wasiwasi wao kuhusu ripoti kwamba Marekani ilikuwa ikipanga kupunguza idadi ya wanajeshi wake, jambo lililoonekana kuwashtua.
Mpango huo wa Trump uliibua maswali kuhusu kujitolea kwake kwa ushirikiano wa muda mrefu na washirika wake wa Ulaya pamoja na katika muungano wenyewe wa kijeshi wa nchi za magharibi.
Uhusiano mbaya kati ya Trump na Merkel
Trump amesema kuwa Ujerumani ambayo inaongoza kiuchumi katika Umoja wa Ulaya, inapaswa pia kulaumia kwa sababu inaishughulikia Marekani vibaya kibiashara. Ameongeza kuwa kwa sasa wanafanya mazungumzo kuhusu hilo lakini bado hajaridhishwa na mpango wa Ujerumani. "Wametugharimu mabilioni ya dola kwa miaka mingi katika biashara. kwa hivyo tunaumia katika biashara na pia kuhusu NATO" Amesema Trump.
Hapo nyuma, Rais Trump hajakuwa na uhusiano mzuri na kansela wa Ujerumani Angela Merkel. Wiki chache zilizopita, tofauti kati yao ilijitokeza wakati Angela Merkel alikataa wito wa kuhudhuria mkutano wa kilele wa kundi la G7 mjini Washington, akitaja janga la corona kuwa sababu kwa kulazimisha safari nyingi kusitishwa.
Chanzo: AFPE