Trump kutembelea mji wa Kenosha licha ya kukataliwa
1 Septemba 2020Kenosha ni eneo linaloangaziwa nchini Marekani kutokana na maandamano makubwa ya kutisha yaliyofuatia tukio la hivi karibuni la kuyetuliwa risasi na polisi mwanamme Mmarekani mweusi. Rais Donald Trump ameshapewa onyo na kutahadharishwa kwamba hatakiwi katika eneo hilo lakini amezipuuza tahadhari zote na leo anakwenda kwenye eneo hilo.
Wakati akitembelea jimbo muhimu la uchaguzi la Wisconsin, rais huyo wa Marekani anasema hana mipango ya kukutana au kuzungumza na familia ya kijana Jacob Blake mwenye umri wa miaka 29 aliyepigwa risasi na polisi mgongoni mara kadhaa huku watoto wake watatu wadogo wakimtizama kutokea ndani ya gari.
Rais huyo wa Marekani badala yake amesema kinachompeleka Kenosha ni kukutana na maafisa wa polisi na kutazama hasara iliyosababishwa na vurugu zilizozuka katika eneo hilo baada ya Blake kupigwa risasi na polisi wakizungu mnamo Agosti 23.
Soma pia: Trump atumia hotuba ya kukubali uteuzi kumshambulia Biden
Tukio hilo lilimuacha kijana huyo Mmarekani mweusi kupooza katika maeneo ya kuanzia kiunoni kwenda chini na kusababisha mji mzima kuingia kwenye vurugu kubwa.
Utawala uliogubikwa na mitizamo ya ubaguzi wa rangi
Katika kipindi cha utawala huu wa Trump ambacho kimegubikwa na mivutano ya hisia na mitizano ya ubaguzi wa rangi,Kenosha umeshuhudia maandamano makubwa ya kupigania haki za watu weusi yaliyopewa jina ya Black Lives Matter,vurugu,kupelekwa kwa wanajeshi,askari wakizungu ambapo pia tukio hilo lilichangia kijana wa miaka 17 mwanamgambo Kyle Rittenhouse kudaiwa kuwapiga risasi na kuwauwa watu wawili katika maandamano na kumjeruhi mmoja.
Soma pia: Maoni: Trump anaweza kushinda vita hii
Wanademocrats pamoja na watetezi wanaodai mageuzi katika idara ya polisi wanauona mji wa Kenosha kama alama ya ubaguzi wa rangi uliojengeka kama tabia ya kawaida katika taasisi,hali ambayo inasababisha matukio ya vurugu za umwagikaji wa damu kati ya maaskari polisi na washukiwa ambao ni watu weusi.
Wanamtazama kijana Rittenhouse ambaye ni mfuasi sugu wa rais Trump kama nembo ya wanamgambo wa siasa kali za mrengo wa kulia ambao wanazidi kuonesha ushabiki wa silaha katika mifumo ya kisiasa na kujaribu kujionesha kama walinda usalama wasiolipwa.
Rais Donald Trump amekataa katakata kulaani mauaji yaliyofanywa na Rittenhouse aliyekuwa akizunguuka akiwa amekamata bunduki.
Soma pia: Michelle Obama asema Trump hafai kuiongoza Marekani
Hata hivyo rais huyo wa Marekani ameweka wazi kwamba anakwenda Kenosha akiwa na mtazamo tafauti alioupa kipaumbe ambao unahusu kile alichokuwa anakisema mara kwa mara yaani uvunjivu wa sheria anaodai unaotokana na ukosefu wa mamlaka katika miji inayoongozwa na chama cha Democratic.