Trump: Maandamano ya mjini Kenosha ni 'ugaidi wa ndani'
2 Septemba 2020Rais Donald Trump Jumanne alipeleka ujumbe wake makhsusi wa kusisitiza kuzingatia sheria katika jiji la Kenosha, ambapo aliyaelezea maandamano ya hivi karibuni ya kupinga ubaguzi wa rangi kuwa ni vitendo vya ugaidi wa ndani ya nchi vinavyofanywa na makundi ya watu wanaopendelea kuzusha vurugu.
Rais Trump anasema kusudio la safari yake hiyo lilikuwa kujionea yaliyotokea na pia kuwashukuru polisi kwa kuilinda jamii. Alisema ili kumaliza vurugu lazima tukabiliane na matendo yote yanayohusiana na itikadi kali, na hapo hapo akawalaumu wanasiasa wanaotoa ujumbe unaosababisha madhara. Katika mkutano huo Mwanasheria Mkuu William Barr, kaimu Katibu wa Idara ya Usalama wa Taifa Chad Wolf, na wachungaji wa kanisa analohudhuria mama yake Jacob Blake walikuwepo kwenye ukumbi huo.
Rais Trump binafsi hakuzungumza na familia ya Blake lakini alisema anasikitishwa sana na matukio kama hayo kwa mtu yeyote yule. Alimpongeza mkuu wa polisi wa jiji la Kenosha David Beth, ambaye anakosolewa kwa kauli aliyotoa juu ya kuwahifadhi watu wanaoshukiwa kuhusika katika uhalifu ili wasiweze kuzaa tena.
Wanachama wa chama cha Democratic na watetezi wanaotaka mageuzi kwenye idara ya polisi wanauona mji wa Kenosha kama ishara ya taasisi ya ubaguzi wa rangi. Trump, hata hivyo ana kipaumbele tofauti, anapinga kile ambacho amekielezea mara kwa mara kama machafuko katika miji inayoongozwa na Wademocrat. Amesema Wamarekani wanapaswa kulaani kauli kali dhidi ya polisi.
Gavana wa jimbo la Wisconsin na meya wa Kenosha, wote wa chama cha Democratic, walimsihi Trump asiutembelee mji huo lakini alipuuza ombi lao. Joe Biden amemlaumu rais Trump kwa kuchochea ghasia kwa makusudi ili kujinufaisha kisiasa. Vurugu za wiki iliyopita huko Kenosha zilikumbushia maandamano ya miezi kadhaa ya kuwapinga polisi na ubaguzi wa rangi, yaliyosababishwa na kifo cha Mmarekani mweusi George Floyd ambaye hakuwa na silaha. Alikufa mikononi mwa polisi katika mji wa Minneapolis.
Vyanzo: AFP/DW