1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump: Marekani itaiuzia India silaha za kijeshi

Angela Mdungu
25 Februari 2020

Rais Donald Trump wa  Marekani anahitimisha ziara yake hii leo nchini India wakati mataifa hayo mawili yakiwa  katika juhudi za kukuza mahusiano ya kibiashara

Indien Staatsbesuch von Donald Trump in Neu Dehli
Picha: AFP/P. Singh

Katika hotuba yake ya leo Trump amesema, nchi hizo mbili zimefanya mazungumzo na India itanunua silaha za kijeshi kutoka nchini mwake.

Baada ya mazungumzo na Waziri mkuu wa India Narendra Modi, Rais Trump amesema ziara yake nchini humo imekuwa ya manufaa baada ya makubaliano ya kuiuzia India silaha za kijeshi zikiwemo helikopta za  Apache na Romeo MH-60 alizoziita bora zaidi duniani.

Katika hotuba yake hiyo ameongeza kuwa yuko tayari kuwa msuluhishi wa mgogoro kati ya India na Pakistan kuhusu jimbo la Kashmir. Awali katika siku yake ya pili na ya mwisho ya ziara yake nchini humo Trumpalihudhuria hafla iliyofanyika kwa heshima yake mjini New Delhi. Katika siku ya kwanza ya ziara yake jana Jumatatu, Trump alihutubia mbele ya zaidi ya raia 100,000 wa India mjini Ahmedabad, ambapo kati ya mambo mengi aliisifu nchi hiyo kwa kuwa na demokrasia yenye mafanikio. 

Kwa upande wake waziri mkuu wa India Narendra Modi amesema mazungumzo ya kulegeza mvutano kati ya India na Marekani yataendelea. Mvutano wa kibiashara baina ya nchi hizo mbili uliibuka baada ya utawala wa Trump kupandisha viwango vya ushuru kwa chuma na aluminium zinazoingia Marekani kutoka India. Taifa hilo nalo lilijibu kwa kuzitoza ushuru mkubwa bidhaa za kilimo na kuweka vikwazo kwa vifaa vya hospitali vya Marekani.

Rais Donald Trump akiwa na mwenyeji wake waziri mkuu wa India Narendra ModiPicha: AFP/M. Ngan

Wakati huohuo, vurugu zinazotokana na maandamano zimeibuka upya katika mji mkuu wa India New Delhi leo, siku moja baada ya watu saba kujeruhiwa akiwemo afisa wa polisi kutokana na makabiliano baina ya watu wanaounga mkono na wale wanaopinga sheria mpya ya uraia ya nchi hiyo.

Polisi nchini humo walilazimika kutumia mabomu ya gesi ili kuwatawanya waandamanaji hao. Sheria inayosababisha vurugu hizo inatajwa kuwapatia msamaha wahamiaji ambao si Waislamu kutoka nchi tatu za jirani ambako wasio waislamu ni wachache. Nchi hizo ni Pakistani, Bangladeshi na Afghanistani.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW