1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump: Marekani na EU zinashughulikia mvutano wa kibiashara

Caro Robi
9 Juni 2018

Rais wa Marekani Donald Trump katika mkutano wa G7, amesema kwa miaka mingi, nchi yake imekuwa ikipata nakisi kubwa inapofanya biashara na Umoja wa Ulaya ila sasa wanalishughulikia suala hilo.

Kanada G7 Gipfel
Picha: picture-alliance/AA/E. Bolte

Amesisitiza kuwa Marekani na washirika wake wa Ulaya hukabiliwa na changamoto kidogo wakati mmoja au mwingine linapokuja suala la biashara lakini pande zote mbili zinafanya mazungumzo.

Trump aliyekutana na Macron jana jioni ameongeza kusema kuwa Marekani na nchi za Umoja wa Ulaya zimekuwa na uhusiano mzuri na wa kipekee na anatumai watapata matokeo chanya kuhusiana na mvutano huo wa kibiashara, uliojitokeza baada ya Marekani kuziongezea kodi bidhaa za chuma na bati za Umoja wa Ulaya.

Je, muafaka utapatikana G7?

Kwa upande wake, Macron amesema mazungumzo yanayoendelea katika mkutano huo wa kilele wa G7 yanaonesha dalili za pande zote husika kuwa na utayari wa kufikia makubaliano yatakayowanufaisha wote.

Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Reuters/K. Lamarque

Trump aliwasili Canada kuhudhuria mkutano huo wa G7 akiwa ameshikilia msimamo wake kuwa maamuzi aliyoyachukua kuhusiana na biashara kati ya nchi yake na nchi sita wanachama wa G7 yanafaa ili kuzilinda kampuni na biashara za Marekani dhidi ya ushindani usiofaa wa kibiashara.

Kuongeza hali tete iliyopo katika mazingira ya mkutano huo wa siku mbili unaokamilika leo Jumamosi, kiongozi huyo wa Marekani amependekeza Urusi inapaswa kurejeshwa katika kundi hilo la nchi zilizoendelea zaidi duniani kiviwanda.

Urusi ilifurushwa kutoka kundi hilo mwaka 2014 baada ya kuichukua rasi ya Crimea kutoka Ukraine. Wito huo wa Trump uliungwa mkono na waziri mkuu mpya wa Italia Giuseppe Conte lakini viongozi wengine waliweka wazi kuwa Urusi haikaribishwi kujiunga tena na kundi hilo la G7.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema Urusi haiwezi kurejeshwa katika kundi hilo hadi ifanye kile alichokitaja hatua za tija kuhusiana na mzozo wa Ukraine, mtazamo unaoungwa mkono na Ufaransa na Canada.

Msemaji wa Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema kujiunga tena na  G7 sio suala wanalolitilia maanani na kwamba kwa sasa nchi hiyo inaelekeza juhudi zake kwingine.

Suala hilo la Urusi linatishia kugubika suala kuu ambalo ni vita vya kibiashara vinavyonukia kati ya Marekani na washirika wake. Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk amesema msimamo wa Trump unawakilisha changamoto kwa sheria za kimataifa kuhusu biashara.

Mahusiano tete kati ya Marekani na EU

Trump pia alikutana na mwenyeji wa mkutano huo wa G7, Waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau. Rais huyo wa Marekani amesema Canada na Marekani zinajaribu kufikia makubaliano ya kupunguza  kodi na vizingiti vya kibiashara na amemueleza Trudeau kuwa anaamini mahusiano kati ya nchi zao yameboreka zaidi wakati huu kuliko wakati mwingine ule.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Reuters/Y. Herman

Trudeau na Macron ndiyo wanaoongoza kampeini ya kupinga nyongeza ya ushuru iliyotangazwa na Trump. Licha ya mazungumzo magumu, wanadiplomasia wameyataja majadiliano yanayoendelea kuwa ya kirafiki na yenye tija.

Ikulu ya White House imetangaza Trump ataondoka mapema kutoka katika mkutano wa G7 kuekelea Singapore kwa ajili ya mkutano ujao wa kilele kati yake na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un kuhusiana na kusitishwa mpango wa kinyuklia wa Korea Kaskazini.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas ameliambia gazeti la Sueddeutsche Zeitung kuwa kuna tofauti kati ya Marekani na washirika wake ambazo amezitaja haziwezi tena kufagiwa na kuwekwa chini ya zulia.

Maas amesema Trump kujiondoa kutoka mkataba wa kuyalinda mazingira wa Paris, makubalino kuhusu mpango wa kinyuklia wa Iran na kuziongezea ushuru nchi washirika yote ni maamuzi ambayo yanaiathiri vibaya Ulaya.

Mwandishi: Caro Robi/dpa/afp/Reuters

Mhariri: Sekione Kitojo