Trump, May wafanya mazungumzo ya kibiashara
4 Juni 2019Akizungumza katika mkutano ambao unaendelea kwa sasa na viongozi wa kibiashara, Trump amemuwambia May kuwa Marekani inaweza kufikia makubaliano muhimu na ya haki na Uingereza baada ya kukamilika mchakato wa Brexit. Rais huyo wa Marekani amemshukuru May kwa kufanya kazi nzuri zaidi na hata akamuomba waziri huyo mkuu aendelee kuwepo ili wakamilishe muafaka huo kabla ya kuachia wadhifa wa waziri mkuu.
Ziara ya Trump ya siku tatu kimsingi inaingiliana na kumbukumbu ya kesho Jumatano ya miaka 75 ya operesheni ya kumalizika kwa vita kuu ya pili ya dunia. Maarufu kama D-Day.
Lakini inakuja hasa katika wakati mgumu kwa Uingereza. May atajiuzulu kama koongozi wa chama cha Conservative Ijumaa baada ya kushindwa kufanikisha mpango wa nchi hiyo kujiondoa katika Umoja wa Ulaya – Brexit.
Ataendelea kuwa waziri mkuu hadi mrithi wake atakapopatikana miongoni mwa wagombea 13 ambao lazima wachukue maamuzi magumu kabla ya muda wa mwisho uliochelewesha mara mbili wa Brexit, ambao ni Oktoba 31.
Trump tayari amelizungumzia suala la Brexit kwa kuiomba Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya bila ya makubaliano – na akadokeza kuwa aliyekuwa waziri wa mambo ya kigeni Boris Johnson ambaye anaunga mkono Brexit, anaweza kuwa chaguo bora zaidi la kuiongoza serikali na kukamilisha suala hilo.
Mazungumzo hayo ya asubuhi yamehudhuriwa na waziri wa fedha wa Uingereza Philip Hammond na waziri wa biashara za kimataifa Liam Fox. Ujumbe wa Marekani unajumuisha waziri wa mambo ya Nchi za Kigeni Mike Pompeo na Waziri wa Fedha Steven Mnuchin.
Wakati wa mazungumzo hayo, kulikuwa na maandamano yenye kelele mitaani yaliyofanywa na maelfu ya watu wanaompinga Trump. Waandamanaji walibeba sanamu kubwa la mpira lenye sura ya Trump na rangi ya chungwa.
Miongoni mwa wanaoshiriki ni wanaharakati wa mazingira, wanaopinga ubaguzi na waandamanaji wanaounga mkono haki za wanawake.
Kiongozi wa chama cha upinzani cha Labour Jeremy Corbyn anatarajiwa kuzungumza katika maandamano hayo. Hapo jana alisusia hafla ya chakula cha jioni katika Kasri la Buckingham iliyoandaliwa na Malkia Elizabeth II, kama hatua ya kulalamikia sera za Trump.
Alisema maandamano ya leo ni fursa ya kuonyesha mshikamano na wale ambao Trump amewashambulia nchini Marekani, kote duniani na pia nchini Uingereza.
May na Trump watakamilisha ziara hiyo kwa kuungana na viongozi wengine wa ulimwengu hapo kesho katika bandari ya Uingereza ya Portsmouth katika kumbukumbu ya miaka 75 tangu wanajeshi wa Uingereza, Marekani na washirika wengine walipoanza operesheni ya kuikomboa Ulaya mnamo Juni 6, 1944 kutoka mikononi mwa Manazi.